Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MBARALI WAMPONGEZA RAIS SAMIA KUSOGEZA KARIBU HUDUMA ZA UPASUAJI MTOTO WA JICHO

Posted on: August 17th, 2023

Na. Majid Abdulkarim, Mbarali

Wananchi wa Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwasogezea huduma za upasuaji wa mtoto wa jicho karibu na kuwaondolea tatizo la upofu.

Hayo yamebainishwa na mmoja wa wagonjwa ambaye amefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho Bi. Sabina Sent (65) kupitia kambi ya siku saba ya Madaktari Bingwa wa upasuaji wa macho Wilayani humo chini ya ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Helen Keller.

“Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia matibabu ya macho bila malipo, nimekuja nikiwa sioni lakini sasa naweza kuona vizuri macho yangu yote”, ameeleza Bi. Sabina.

Bi. Sabina amesema kuwa amekuwa haoni kwa muda wa miaka miwili lakini baada ya kufika katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali na kufanyiwa uchunguzi kisha upasuaji anarudi kwake akiwa na tabasamu la kuona.

Kwa upande wake Mzee Richard Enock (59) amesema ameishi na tatizo la kutokuona kwa miaka 18 lakini leo baada ya kufanyiwa upasuaji na madaktari bingwa wa macho bila malipo anaweza kuona vizuri.

Mzee Enock ameeleza kuwa tatizo la kutokuona lilimuanza toka mwaka 2005 ambapo lilianza jicho moja na kila siku nguvu ya kuona ikawa inapungua mpaka macho yote yakawa hayaoni tena.

“Namshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kutujali sisi wananchi kwa kutusogezea huduma za macho karibu na sisi maana sikuwa na uwezo wa kusafiri kufata huduma hizi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya”, amesema Mzee Enock

Naye Mtoto wa mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho, Nassoro Atupele amesema kuwa amefarijika sana kuona baba yake anaona kwani amekuwa haoni tangu mwaka 2014 ndo alipata tatizo la mtoto wa jicho na kuacha kuona kabisa.

“Nitoe wito kwa shukrani zangu za dhati kwa Serikali yetu, pia naomba huduma hizi ziwe ni endelevu kwani sio kila Mtanzania ataweza kusafiri kufika Hospitali zinazotoa huduma hizi za upasuaji kama zilivyotufata hapa Mbarali”, amesisitiza Atupele