MAWAZIRI WA AFYA WA EAC WARIDHIA TANZANIA KUWA MWENYEJI WA VITUO VIWILI VYA UMAHIRI VYA KIKANDA
Posted on: May 9th, 2025
Mawaziri wa Afya kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana jijini Arusha katika Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya na kuridhia rasmi uanzishwaji wa Vituo viwili vya Umahiri vya Kikanda nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel na kiongozi wa ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono ajenda ya afya ya EAC kwa kuimarisha mifumo ya afya, kuwekeza katika rasilimali watu na miundombinu ya afya ili kwenda sambamba na vipaumbele vya kitaifa na kikanda.
Uamuzi huo umetokana na mapendekezo yaliyowasilishwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kuanzishwa kwa Kituo cha Umahiri cha Sayansi ya Afya ya Kinywa na Meno kitakachokuwa chini ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto na Sayansi ya Magonjwa ya Damu kitakachokuwa chini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Pia Dkt. Mollel amesisitiza kuanzishwa kwa vituo vya umahiri ni hatua muhimu katika kuongeza uwezo wa huduma za afya maalum ndani ya kanda.
Katika kukabiliana na changamoto mpya za kiafya kama ugonjwa wa Mpox, Dkt. Mollel ametoa wito kwa nchi wanachama kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa, kuboresha maabara na kuongeza ushirikiano katika maeneo ya mipakani.
Aidha amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii na mawasiliano sahihi katika kupambana na upotoshaji na unyanyapaa unaohusiana na magonjwa na azma ya Tanzania kuendeleza elimu ya tiba kupitia miradi na program za kikanda na juhudi za kuoanisha mitaala ya tiba na udaktari katika Jumuiya.