MATIBABU YA KIBINGWA YA MADAKTARI WA DKT. SAMIA UKOMBOZI KWA WANANCHI SONGWE
Posted on: September 17th, 2025
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Jabiri Omari Makame leo Septemba 15, 2025 amezindua rasmi huduma mkoba za Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia mkoani Songwe ikiwa ni juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia wananchi wote kwa ukamilifu.
Katika hotuba yake, Mhe. Jabiri Makame ameeleza kuwa ujio wa kambi hiyo ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia ni ishara ya dhamira ya dhati ya Serikali ya kuimarisha huduma za afya mkoani Songwe.
Amebainisha kuwa kuanzia mwaka 2020 hadi 2025, mkoa umepata maendeleo makubwa ikiwa ni pamoja na ongezeko la vituo vya afya kutoka 205 hadi 273, na hospitali kutoka 2 hadi 5, vyote kwa lengo la kuboresha huduma za msingi na za kitaalam kwa wananchi.
“Serikali imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 40.6 kwa ajili ya kuboresha miundombinu, ununuzi wa dawa, vifaa, na vitendanishi, pamoja na kuanzisha afua mbalimbali za tiba ikiwemo lishe, kudhibiti malaria, kifua kikuu, na magonjwa ya zinaa na UKIMWI. Kupitia juhudi hizi, upatikanaji wa dawa umeongezeka kwa asilimia 90, hali inayorahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka 320 mwaka 2022 hadi 146 mwaka 2023, mkoa umepokea watumishi wa sekta ya afya 725 kuanzia mwaka 2021 hadi 2025, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na upungufu wa watumishi wa afya, na kufanya huduma kuwa karibu zaidi kwa wananchi,” amesema Mhe. Jabiri Makame
Aidha Mhe. Jabiri Makame, ametoa rai kwa viongozi na watendaji wa mkoa kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa karibu kwa madaktari ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinafikia viwango vya juu na wananchi wanafaidika kwa kiwango cha juu.