Ministry of Health

MAFUNZO YA RRT KUTOA MSUKUMO KATIKA KUDHIBITI MAJANGA YA DHARURA NA MAGONJWA YANAYOZUILIKA KWA CHANJO

Posted on: May 18th, 2026

Na Andrea Kadege, WAF-Mwanza

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Gabriel Mashauri amesema kuwa mafunzo yanayotolewa kwa timu za haraka za kukabiliana na Majanga ya Dharura ni muhimu katika kutoa msukumo katika kudhibiti Dharura za kiafya na Magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

Dkt. Gabriel Mashauri amesema hayo leo Mei 18, 2026 Mkoani Mwanza wakati wa kufungua kikao kazi cha mafunzo hayo huku akihimiza kuwa uwepo wa timu hizo katika Mikoa ni jambo muhimu kwani Mwanza ni Mkoa wenye muingiliano mkubwa wa watu kutoka Mataifa mbalimbali ikiwepo Kenya na Uganda hivyo timu hizo ni muhimu katika kukabiliana na dharura za kiafya pindi yakitokea.

Dkt. Mashauri amewataka wataalam hao kuzingatia mafunzo wanayopewa kwani ni mkakati wa kuhakikisha afya za Watanzania zinalindwa muda wote kwa maslahi mapana ya Taifa.

Aidha, amewataka Wataalam hao kuhakikisha wanakuwa daraja la kutoa ujuzi kwa Wataalam wengine katika ngazi za msingi ili wananchi wawe na uelewa mpana wa kuchukua hatua stahiki pindi majanga yanapotokea huku akisisitiza kuwa, hatua muhimu zitachukuliwa kwa Wataalam kupima matokeo ya mafunzo waliyopewa jinsi yanavyosaidia jamii.

Naye Dkt.Simon Chacha kutoka Wizara ya Afya Idara ya Dharura na Maafa, ameeleza kuwa Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa Mikoa 11 ambayo Wizara ya Afya inaitambua kama Mikoa iliyo katika hatari kubwa ya kukumbwa na majanga ya dharura pamoja na magonjwa ya mlipuko, hivyo ni muhimu kwa timu za kukabiliana na majanga kuendelea kujengewa uwezo wa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza

"Mkoa wa Mwanza umepata fursa ya kipekee kwa sababu mafunzo haya yamefanyika kwa awamu ya pili huku yakihusisha jumla ya Wataalam 75 ambapo idadi imeongezeka kutoka Wataalam 35 waliojengewa uwezo kwa ya awamu ya kwanza na Wataalam 40 katika awamu hii ya pili" amesema Dkt. Chacha

Ameongeza kuwa, mafunzo hayo yanatolewa ikiwa ni mikakati ya kuhakikisha timu hizi katika Mkoa wa Mwanza zinakuwa na uwezo wa kukabiliana na athari zitakazojitokeza kwa uharaka zaidi kabla ya timu za Kitaifa kuja kwa ajili ya kutoa usaidizi zaidi wa Kitaalam.