MAFUNZO YA HUDUMA ZA DHARURA KWA WATAALAM KUSAIDIA KUBORESHA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA KWA WANANCHI
Posted on: April 20th, 2026Na Happyness Hans, WAF – Kigoma
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dkt. Damas Kayela, amesema mafunzo yanayotolewa kwa wataalam wa afya mkoani humo ni fursa muhimu ya kuboresha utoaji wa huduma za dharura, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi na kasi ya kuwahudumia wananchi wanaohitaji msaada wa haraka wa huduma za afya.
Dkt. Kayela ameyasema hayo Aprili 14,2026 mkoani Kigoma, ameongeza kuwa, ujio wa wataalam kutoka ngazi ya Taifa kuanzia Aprili 13 hadi 26, 2026, unalenga kufanya tathmini ya kina katika sekta ya afya ili kubaini mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zilizopo katika utoaji wa huduma ya afya.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya wataalam wa ngazi ya Taifa na wale wa mkoa utasaidia kuimarisha maeneo yenye mafanikio na kutafuta suluhisho la changamoto zilizopo, jambo litakaloboresha zaidi huduma za dharura kwa wananchi.
“Ninashukuru kwa ujio wa wataalam kutoka ngazi ya Taifa, tutashirikiana nao kwa karibu kuhakikisha wanabaini maeneo yenye mafanikio na changamoto, ili kwa pamoja tuweze kuboresha huduma na kuendeleza yale mazuri huku tukitatua changamoto zilizopo,” amesema Dkt. Kayela.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Maweni, Dkt. Joseph Nangawe, amesema wamepokea ugeni uliotoa mafunzo kwa wataalam wa hospitali hiyo kuhusu utoaji wa huduma za dharura, amesema mafunzo hayo yamewasaidia kubaini mafanikio yaliyopo pamoja na changamoto zinazohitaji maboresho.
Aidha, ameeleza kuwa uongozi wa hospitali ya Maweni utaendelea kusimamia utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa ili kuboresha maeneo yenye changamoto na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi na kuzingatia ubora.