Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MADAKTARI BINGWA WAREJESHA TABASAMU BAADA YA UPASUAJI WA JIPU

Posted on: October 16th, 2025

NA WAF – SHINYANGA

Bi. Godlive Kalifa, Mkazi wa Shinyanga amepata nafuu na kurejesha tabasamu lake baada ya kufanyiwa upasuaji wa jipu kwenye jino na madaktari bingwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Uso, Kinywa na Mataya kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dkt. Arnold Augustino, amesema hayo leo Oktoba 15, 2025 katika hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga katika kambi ya madaktari bingwa wa Rais Samia.

"Tatizo hili ni hatari sana inaweza kukatisha uhai wa mtu, tumefanikiwa kufanya upasuaji wa uso kwa ajili ya kutoa usaha wa Jipu kwenye jino kutoka kwa binti huyu na sasa anaendelea vizuri," amesema Dkt. Arnold.

Aidha, Dkt. Augustino amesema Serikali imeimarisha huduma za kinywa na meno kwa kuongeza madaktari bingwa, vifaa tiba, na vituo vya huduma katika mikoa na halmashauri, kuhakikisha wananchi wanapata matibabu kwa wakati.

"Nawashauri watu wote kuzingatia usafi wa kinywa ili kujiepusha na matatizo ya kinywa na meno ikiwemo jipu kwenye jino kwani inaweza kuhatarisha maisha pindi unapochelewa kupata huduma za kimatibabu,” amesema Dkt. Anorld.

Kwa upande wake Daktari wa Kinywa na Meno wa hospitali hiyo, Dkt. Godfrey Mushi, ameomba huduma za kupelekewa madaktari bingwa ziwe endelevu kwasababu ni chachu ya kujifunza zaidi pamoja na kupata uzoefu kutoka kwa madaktari hao.