MADAKTARI BINGWA WAFANIKIWA KUONDOA JIWE KWENYE KIBOFU CHA MKOJO
Posted on: October 16th, 2025
NA WAF – SHINYANGA
Timu ya Madaktari Bingwa imefanikiwa kufanya upasuaji kwa Bw. Ramadhan Bilali, mkazi wa shinyanga mwenye umri wa miaka 55, na kuondoa jiwe kwenye kibofu cha mkojo lililomsumbua kwa miaka sita bila kupata ufumbuzi.
Akizungumza leo Oktoba 16, 2025, Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dkt. Joachim Kisaka, amesema upasuaji huo umefanyika katika hospitali ya Ushetu, mkoani Shinyanga, kupitia Kambi ya Madaktari Bingwa.
Dkt. Kisaka amesema kuwa mgonjwa huyo amekuwa akitafuta tiba katika hospitali mbalimbali kwa gharama kubwa bila mafanikio. Baada ya kufanyiwa upasuaji huo, anaendelea vizuri na hali yake inaimarika kwa kasi.
Aidha, Dkt. Kisaka amebainisha kuwa upasuaji huo ni miongoni mwa huduma muhimu zinazotolewa na madaktari bingwa katika kambi hiyo.
Kwa upande wake, Bw. Bilali aliyepatiwa huduma hiyo, ametoa shukrani za dhati kwa madaktari bingwa hao kwa huduma bora alizopatiwa, na kusema kuwa sasa anajisikia nafuu kubwa baada ya mateso ya muda mrefu.
Huduma hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi, ili kupunguza gharama na changamoto za kufuata matibabu mbali na makazi yao.