Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MADAKTARI BINGWA WA SAMIA WAFANYA UPASUAJI KWA MARA KWANZA RORYA

Posted on: November 15th, 2024

Na WAF - RORYA

Jopo la Madaktari Bingwa wa Rais Samia walioweka kambi katika Hospitali ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara wamefanikiwa kufanya upasuaji mkubwa wa kwanza kwa mama mjamzito aliyekuwa na kovu la upasuaji uliotokana na uzazi pingamizi (previous scar).

Upasuaji huo umefanyika Novemba 13, 2024 katika Hospitali mpya ya wilaya ya Rorya, ambapo madaktari hao walifanya upasuaji kwa mama huyo na kufanikiwa kupata mtoto wa kiume akiwa na afya njema.

Upasuaji huo uliongozwa na Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dkt. Halima Basila kutoka hospitali ya Nyamagana mkoani Mwanza kwa kushirikiana na Daktari Bingwa wa Usingizi na Ganzi, Dkt. Benard Kenemo kutoka hospitali ya rufaa ya kanda Bugando pamoja na Muuguzi Mbobezi Bi. Lilian Mushi kutoka hospitali ya Serian Arusha na wanataaluma wengine wa hospitali ya Rorya.

Uwepo wa vifaa tiba vya kutosha umerahisisha zoezi hili na kuanzia sasa akina mama watakuwa wanapata huduma hiyo katika hospitali hiyo ya wilaya ya Rorya na itapunguza adha ya wakina mama kufuata huduma ya upasuaji Musoma mjini umbali usiopungua kilomita 45 lakini pia kuepusha vifo.

Madaktari bingwa wamekuwa wakitoa huduma pamoja na kuwajengea uwezo watumishi katika hospitali hiyo, ambapo kampeni hii ya madaktari bingwa wa Rais Samia imekua na umuhimu mkubwa katika kuboresha afya za wananchi na kupunguza adha kwa maradhi yanayohitaji huduma za kibingwa.