MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WATOA HUDUMA ZA KIBINGWA NA UBOBEZI KAGERA
Posted on: April 28th, 2025
Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi wa Rais Samia wameanza kambi rasmi ya utoaji huduma za kibingwa katika halmashauri zote nane (8) za mkoa wa Kagera, lengo likiwa kupeleka huduma hizo kwa wananchi na kuwapunguzia gharama za matibabu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa zoezi hilo leo Aprili 28, 2025 Mkuu wa Wilaya Bukoba Mhe. Erasto Sima amesema mkoa wa Kagera umekuwa ukitumia gharama kubwa kwa ajili ya rufaa za wagonjwa kuelekea hospitali kubwa za Bugando na Chato lakini uwepo wa madaktari hao katika hospitali za mkoa na wilaya unaleta nafuu kubwa ya gharama za matibabu ya huduma za kibingwa.
Mkuu huyo wa Wilaya amefungua zoezi hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Fatuma Mwasa na amewahakikishia madaktari hao kuwa kutakuwa na magari ya wagonjwa ya kutosha kwa ajili ya kutoa huduma kwa wale wagonjwa watakaohitaji huduma hiyo.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amewaeleza Madaktari Bingwa wa Rais Samia kuwa pamoja na changamoto zilizopo, mkoa wa Kagera umeendelea kuboresha huduma za Afya ya Uzazi na Watoto akibainisha kuwa takribani asilimia 90 ya akina mama wamehudumiwa katika vituo vya kutolea huduma kwa mwaka 2024.
Amezitaja changamoto zilizopo katika huduma ya Afya ya Uzazi na Watoto kuwa ni upungufu wa watumiushi wenye ujuzi, upungufu wa vifaa tiba, magari ya kubebea wagonjwa wanaohitaji rufaa, miundombinu ya barabara na upungufu wa damu salama.
Huduma za kibingwa zitakazotolewa katika zoezi hili litakalohitimishwa Mei 3, 2025 ni huduma za ubobezi wa watoto wachanga, magonjwa ya wanawake na ukunga, upasuaji bobezi wa mfumo wa mkojo, ubingwa wa usingizi na ganzi, magonjwa ya ndani, meno na wauguzi wakunga wabobezi.