Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MADAKTARI BINGWA WA RAIS DKT. SAMIA KUWEKA KAMBI YA SIKU SITA MKOANI LINDI

Posted on: September 16th, 2025

Na WAF, Lindi


Kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan awamu ya nne (4) imeanza rasmi mkoani Lindi, kwa kupokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bi. Zuwena Omari.


Akizungumza leo Septemba 15, 2025 wakati wa mapokezi, Katibu Tawala amesisitiza umuhimu wa kambi hiyo akieleza kuwa inaleta ahueni kwa wananchi na kuwaepusha kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibingwa.


“Zoezi hili ni zuri kulingana na uwekezaji wake, uwepo wake unasaidia wananchi kupata huduma katika maeneo yao ya karibu. Wito wangu  tuendelee kutumia fursa hii, na kila mwenye changamoto afike katika vituo vya kutolea huduma za afya, tuko pamoja,” amesema Bi. Zuwena.


Jumla ya wataalam mabingwa 47 watatoa huduma katika kambi hiyo, wakiwemo wa magonjwa ya ndani, usingizi, upasuaji, meno, watoto, pamoja na wanawake na uzazi, ambapo watatoa huduma katika halmashauri zote saba (7) za mkoa wa Lindi.



Kambi hiyo inalenga kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi wa mkoa wa Lindi, ikiwa ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi wote nchini.