MADAKTARI BINGWA WA DKT. SAMIA WAOMBWA KUTOA UJUZI KWA WATAALAM WA VITUO
Posted on: June 9th, 2025
Na WAF - DSM
Madaktari Bingwa wa Rais Samia pamoja na kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi pia wametakiwa kuwajengea uwezo wataalam wanaowakuta kwenye vituo walivyopangiwa.
Hayo yamesemwa Juni 09, 2025, na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila wakati akiwapokea madaktari bingwa wa Dkt. Samia watakaotoa huduma kwa muda wa siku sita katika Hospitali tano za Halmashauri za jiji hilo.
Mhe.Mpogolo ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kufadhili program hiyo ya Madaktari bingwa wa Samia ambao wameendelea kutoa huduma za kibingwa na bobezi katika Hospitali za Halmashauri na Wilaya nchi nzima.
"Nawaomba Madaktari ambao mmepangwa kutoa huduma za ubingwa na bobezi katika Hospitali mbalimbali za Wilaya kwenye mkoa wetu wa Dar es Salaam, mkawe chachu na hamasa ya kujifunza kwa wataalam mtakaowakuta ili na wao waweze kuwa mabingwa kama nyie kwa kuwashirikisha wakati mkitoa huduma," amesema Mhe.
Mpogolo.
Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wataalam walioko katika hospitali hizo kuwa bega kwa bega na madaktari bingwa ili wajifunze na kutoa huduma bora kwa wananchi watakaofika kupata matibabu.
Aidha, Mhe. Mpogolo amewaomba wananchi wenye shida mbalimbali za kiafya kutumia nafasi hiyo adimu kufika katika hospitali zilizo karibu yao ili kupata huduma za kibingwa kwa gharama nafuu.
Naye mratibu wa zoezi hilo kutoka Wizara ya Afya Bi. Faraja Mgeni ameushukuru Mkoa wa Dar es Salaam kwa mapokezi mazuri ya Madaktari Bingwa hao ambapo mpaka sasa wananchi zaidi ya 154,000 wameshafikiwa kupata huduma za kibingwa katika wilaya 180 za mikoa mbalimbali nchini huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma katika hospitali ambazo madaktari hao watakuwepo.
Madaktari bingwa wa Dkt. Samia katika Mkoa wa Dar es Salaam watahudumia wananchi kwa siku sita kuanzia tarehe 9 hadi 14 Juni 2025 katika hospitali za Kivule, Kigamboni, Mwabepande, Mbagala Rangitatu na Ubungo Kimara.