MADAKTARI BINGWA 33 WASOGEZA HUDUMA ZA KIBINGWA BOBEZI RUKWA
Posted on: December 2nd, 2024Na WAF, SUMBAWANGA
Madaktari Bingwa 33 kutoka Kanda ya Magharibi wameweka kambi ya kutoa huduma za kibingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga kwa ajili ya kuwahudumia wakazi wa mkoa wa Rukwa na mikoa jirani.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Katibu Tawala wa Mkoa, Bw. Msalika Makungu, amesema kuwa huduma hizi zitasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi na kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi ambao kawaida wanahitaji rufaa kwenda maeneo mengine ili kupata huduma za kibingwa.
Bw. Makungu ameongeza kuwa wananchi wa mkoa wa Rukwa wana uhitaji mkubwa wa huduma za kibingwa, amewataka madaktari hao kutoa huduma hizo kwa ufanisi ili kuhakikisha wanapata matibabu bora kwa wakati.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dkt. Ibrahim Isaack, amesema kuwa huduma hii ni fursa nzuri kwa madaktari wa mkoa kujifunza na kuboresha ufanisi wao katika utoaji wa huduma za kibingwa kupitia wataalam hao wanaotoa huduma katika kambi hiyo
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga, Dkt. Ismail Macha, amesema kuwa lengo la zoezi la huduma mkoba ni kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi na kupunguza rufaa za magonjwa ambayo hayana madaktari bingwa. Amewashukuru viongozi wa hospitali za Kanda ya Magharibi, madaktari wa Kanda ya Mbeya, na hospitali ya Benjamin Mkapa kwa ushirikiano wao mkubwa katika kambi hiyo.
Kambi ya madaktari bingwa wa Dkt. Samia Kanda ya Magharibi inaratibiwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni-Kigoma, Kitete-Tabora, na Katavi. Kambi hii ilianza rasmi leo tarehe 2 Desemba 2024 na inatarajiwa kumalizika tarehe 6 Desemba 2024.