Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MAAMBUKIZI MAPYA YA VU YAMEPUNGUA KUTOKA ASILIMIA 7 HADI ASILIMIA 4.3

Posted on: November 7th, 2023


Imeelezwa kuwa kasi ya maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI imepungua kutoka asilimia 7% mwaka 2003 hadi kufikia asilimia 4.3% mwaka 2022.

 

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, akimuwakilisha Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu wakati akiongoza ujumbe wa wageni kutoka Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa UKIMWI ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Msaidizi (PDAS) na Kaimu Naibu Mratibu Mkuu wa masuala ya UKIMWI wa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa UKIMWI (PEPFAR), Dk Rebecca Bunnell ulipotembelea Mkoa wa Tanga katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa Mhe. Waziri Kindamba pamoja na Kituo cha Warahibu wa Dawa za Kulevya "Gift of Hope" kilichopo Jijini Tanga.

 

“Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma za afya, hasa katika huduma jumuishi kwa waathirika wa dawa za kulevya na VVU” amesema Dkt. Magembe.

 

Aidha Dkt. Magembe amesema kupitia ufadhili wa PEPFAR Tanzania imeweza kuanzisha vituo tisa vya utoaji wa dawa ya Methadone kwa waathirika wa dawa za kulevya nchi nzima, pamoja na huduma ya kliniki ya kutembea katika vituo saba.

 

“Tunaishukuru Serikali ya Marekani kwa msaada wake kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa UKIMWI (PEPFAR) kwa kuendelea kushirikiana katika uboreshaji wa huduma za afya nchini na mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi” amesema Dkt. Magembe.

 

Kwa upande wake, Dkt. Rebecca Bunnell ameishukuru Serikali ya Tanzania kumkaribisha kuja kuona shughuli za PEPFAR Mkoani Tanga na pia alishukuru kwa ushirikiano unaonyeshwa na Serikali ya Tanzania katika mapambano ya VVU na UKIMWI nchini.


Dkt. Rebecca amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha huduma za afya nchini na kuahidi kuwa Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha zaidi huduma za Afya.