Customer Feedback Centre

Ministry of Health

KIKAO CHA BARAZA KITOKE NA MAAMUZI YENYE TIJA KWA SEKTA YA AFYA

Posted on: March 12th, 2025

Na WAF - Mwanza

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama alitaka Baraza la watumishi wa Wizara ya Afya na Taasisi zake mijadala yao ilenge kuleta tija na ufanisi ili kuendelea kuinua sekta ya afya nchini.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Machi 12, 2025 wakati akifungua kikao cha Baraza la wafanyakazi la Wizara ya Afya kinachofanyika mkoani Mwanza, chenye lengo la kuwawezesha watumishi kushiriki kikamilifu katika uongozi wa pamoja mahali pa kazi na kuimarisha mahusiano kati ya wafanyakazi na waajiri katika ngazi zote za Wizara.

"Natumaini kuwa maamuzi yatakayofikiwa hapa kwenye kikao chetu muhimu, yatakuwa na mchango mkubwa katika kuinua Sekta ya Afya kwa maslahi mapana ya Wizara na Taifa kwa ujumla, kwa msingi huo, nawasihi tushiriki mijadala yenye tija, tukijadili kwa kina na kwa mtazamo wa kujenga," amesema Waziri Mhagama.

Amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya Mwaka 2002 pamoja na kanuni zake za mwaka 2005, Baraza hilo ni chombo muhimu cha majadiliano na maamuzi yanayolenga kuimarisha mahusiano kati ya wafanyakazi na waajiri katika ngazi zote za Wizara.

Aidha, Waziri Mhagama amesema katika utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2024/25, Wizara imefanikisha utekelezaji wa ufadhili wa masomo kupitia 'Samia Health Specialized program' ambao umewezesha ufadhili wa masomo kwa watumishi wa Sekta ya Afya 544 na kufanya jumla ya watumishi 1,455 kupata ufadhili wa kusomea fani za ubingwa na ubingwa bobezi.

Baraza hilo la wafanyakazi litajadili na kufanya maamuzi kuhusu ajenda kuu tano (5) muhimu ikiwemo kujadili na kupitia utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2024/25, mapendekezo ya Bajeti ya mwaka 2025/26, kupata mrejesho kuhusu rasimu ya miundo ya maendeleo ya utumishi ya kada za Afya.

Awali Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe alisema kikao cha Baraza la Wafanyakazi lipo kwa mujibu wa sheria ili kudumisha mahusiano mema kazini baina ya waajiriwa na muajiri hivyo akawasihi wajumbe kushiriki na kufuatilia mada zote zitakazoletwa mbele yao.