Ministry of Health

KAMATI YAPITIA MATINI ZA ELIMU YA AFYA KWA VIJANA KUPUNGUZA MADHARA YA AFYA YA AKILI

Posted on: June 16th, 2026

Na WAF, Dar es Salaam

Kamati ya Uhakiki wa Vielelezo vya Elimu ya Afya kwa Umma (Content Review Committee - CRC) imepitia matini mbalimbali zitakazotumika kutoa elimu ya afya kwa vijana wenye umri wa miaka 17 hadi 25, walioko katika shule za sekondari, vyuo na makundi mengine ya vijana nchini.

Lengo la mapitio hayo ni kuhakikisha matini hizo zinatoa elimu sahihi itakayosaidia kuwanusuru vijana na madhara yanayoweza kuchangia changamoto za afya ya akili, hususan pale wanaposhindwa kujiepusha na baadhi ya tabia hatarishi zikiwemo matumizi ya dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kikao hicho, wajumbe wamejadili na kuboresha ujumbe wa afya ili kuhakikisha unakuwa rafiki kwa vijana na unaoakisi changamoto halisi zinazowakabili katika jamii.

Akiongea katika kikao hicho kwa niaba ya Katibu wa Kamati, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Afya kwa Umma, Bwana Maxmillian Kwangu, ameipongeza kamati kwa juhudi zake za kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi na yenye tija kwa afya ya wananchi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (HGCU), Bwana Atley Kuni, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usahihi wa taarifa ili kupunguza upotoshaji na taharuki miongoni mwa wananchi, akibainisha kuwa ushirikiano wa wadau ni muhimu ili kufanikisha malengo hayo.

Naye Mratibu wa Kamati hiyo, Bi. Grace Msemwa, amewashukuru wajumbe wote kwa ushiriki wao na mchango wao katika kuboresha matini hizo muhimu kwa jamii.

Kikao hicho kilichoandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kwa ushirikiano na mdau kimehariri jumla ya matini 14, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha vielelezo vinavyotumika kutoa elimu ya afya vinazingatia viwango na miongozo ya kitaifa.