Ministry of Health

KAMATI YA BUNGE YAAGIZA UBORESHAJI WA HUDUMA ZA AFYA NA MIUNDOMBINU HOSPITALINI

Posted on: March 19th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Johannes Lukumay ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Afya kuhakikisha hospitali zote za rufaa nchini zinaweka utaratibu wa kutangaza uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ili kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupata huduma.

Dkt. Lukumay ameyasema hayo leo Machi 18, 2026 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Amesema Kamati imeielekeza Serikali kuangalia namna ya kuongeza watumishi wa sekta ya afya, hususan wataalamu wa ganzi na usingizi, ili kukidhi mahitaji ya utoaji wa huduma za upasuaji na matibabu ya dharura katika hospitali mbalimbali nchini.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kutosha katika vitengo vya huduma za dharura ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka.

Amesema Kamati pia imeelekeza hospitali zote nchini kutenga fedha kupitia mapato ya ndani pamoja na ruzuku ya Serikali kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya hospitali, ikiwa ni pamoja na kuandaa na kutekeleza mipango kabambe (Master Plan) itakayowezesha ujenzi wa majengo ya kisasa ya ghorofa.

Dkt. Lukumay amepongeza kiwango cha usafi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala na kuzitaka hospitali nyingine kuiga mfano huo, huku akisisitiza umuhimu wa kuweka motisha kwa watumishi pamoja na utaratibu wa sare maalum za kazi ili kuongeza nidhamu, usafi na utendaji kazi bora.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya Florence Samizi ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kwa maelekezo yaliyotolewa na kuahidi kuwa Serikali itayafanyia kazi kwa vitendo.

Dkt. Samizi amesema maelekezo hayo yanalenga kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini, na hivyo amewataka watumishi wote wa sekta ya afya kuendelea kufanya kazi kwa weledi, kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi.