Customer Feedback Centre

Ministry of Health

JAMII YATAKIWA KUZINGATIA AFYA YA KINYWA NA MENO.

Posted on: October 16th, 2025

Na, WAF - Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, ametoa wito kwa jamii kuzingatia afya ya kinywa na meno kwani ni viungo muhimu vinavyomsaidia binadamu kujenga afya bora.

Dkt. Shekalaghe ameyasema hayo Oktoba 15, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Kongamano la 15 la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) la usambazaji wa tafiti za afya ya kinywa na meno.

Amesema ni muhimu wananchi kuzingatia ushauri wa wataalam katika kulinda afya ya kinywa na meno, na elimu hiyo inapaswa kuanza majumbani hadi shuleni ili kwa pamoja kulinda afya bora ya jamii.

“Kupitia kongamano hili tumeona jamii inashirikishwa kuhusu masuala ya afya ya kinywa na meno. Tunatafuna chakula na kunywa kwa kutumia kinywa na meno, na chakula hicho ndicho chanzo cha afya njema, hivyo ni vyema kuzingatia ushauri wa wataalam,” amesisitiza Dkt. Shekalaghe.

Aidha, amesema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika huduma za afya ya kinywa na meno kwa kununua vifaa tiba vya kisasa na kuongeza wataalam, hali ambayo imewezesha matibabu ya magonjwa yote ya kinywa na meno kufanyika ndani ya nchi, hivyo kuokoa gharama na muda kwa wananchi.

“Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa Serikali imewekeza katika kada zote za afya, mfano hapa MUHAS sasa wanatoa mafunzo kuanzia ngazi ya stashahada hadi ubingwa bobezi katika kada ya kinywa na meno, jambo linaloonesha Tanzania imepiga hatua kubwa Afrika,” amesema Dkt. Shekalaghe.

Kuhusu mpango wa Bima ya Afya kwa Wote amesema huduma za afya ya kinywa na meno zitajumuishwa katika bima hiyo itakapoanza kutekelezwa.

Kwa upande wake, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Emmanuel Balandya, amesema kongamano hilo litatoa mapendekezo muhimu kuhusu namna ya kuzuia na kutibu magonjwa ya kinywa na meno, huku akibainisha kuwa ushiriki wa Wizara mbalimbali unaonesha dhamira ya Serikali kuyafanyia kazi mapendekezo yatakayotolewa.