Ministry of Health

JAMII YAHIMIZWA KUWEKA MAZINGIRA RAFIKI KWA HEDHI SALAMA KWA WASICHANA NA WANAWAKE

Posted on: March 26th, 2026

Na Said Nyaoza, WAF – Mbeya

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Dkt. Elizabeth Nyema ametoa wito kwa jamii kuweka mazingira rafiki kwa wasichana na wanawake kupata mahitaji muhimu wamati wa hedhi ili kuhakikisha wanakuwa na hedhi salama na yenye staha.

Dkt. Nyema ameyasema hayo leo 25 Machi, 2026 Jijini Mbeya wakati akifunga mafunzo ya usambazaji 'Dissemination' wa Mwongozo wa masuala ya hedhi salama na zana zake katika kanda ya nyanda za juu kusini.

Dkt. Nyema amesema upo umuhimu wa kuwasaidia wanawake na wasichana wakati wa hedhi kwa kuwapunguzia majukumu kwani baadhi yao hupata maumivu makali sana. Alisisitiza uwepo wa Miundombinu muhimu kwa Hedhi Salama ikiwemo Vyoo bora, Maji safi, Sabuni, Taulo za Kike (Pedi) bila kusahau sehemu za kutupia pedi zilizotumika.

"Katika nyakati hizo, ni vyema jamii kwa ujumla ikaona namna ya kumpunguzia mwanamke majukumu ikizingatiwa kuwa majukumu mengi katika ngazi ya familia ikiwemo shughuli za uzalishaji mali na kijamii hutekelezwa na wanawake,"amesema Dkt. Nyema

Pia Dkt. Nyemo amewataka waratibu hao kuhakikisha elimu ya Hedhi Salama inafika kwenye maeneo yote hususani vijijini bila kusahau taasisi kama vile shuleni, si kwa Wasichana na Wanawake tu, bali hata kwa Wanaume na Wavulana.

"Kila mmoja wenu amekabidhiwa nakala ngumu na laini ya Mwongozo sambamba na zana 6 za Hedhi Salama. Nyaraka hizi zisiwekwe kwenye kabati bali zitumike kama rejea ya uchukuaji wa hatua za kurekebisha mapungufu yatakayobainika kuhusu Hedhi Salama," amesema Dkt. Nyemo.

Kwa upande wake Mkuu wa Sehemu Ndogo ya Usalama wa Chakula, Maji na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya, Bw. Anyitike Mwakitalima amesema katika mafunzo hayo jumla ya washiriki 81 kutoka katika halmashauri 34 za mikoa 6 Wamepata mbinu mbalimbali za kufikisha elimu kwa jamii juu ya Mwongozo wa Hedhi Salama na bidhaa zake.

"Hili ni jeshi limeiva na lipo tayari kutoka hapa kwenda kusambaza elimu kuhusu Hedhi Salama, tutakapo kwenda kwenye jamii tukumbuke kutumia lugha fasaha ili kuweza kuendana na mila na desturi zetu bila kumuacha mtu," amesema Bw. Mwakitalima.