IMARISHENI MADAWATI YA HUDUMA KWA MTEJA ILI KUTATUA KERO ZA WANANCHI KWA WAKATI
Posted on: March 28th, 2025
Na WAF - Dodoma
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amewataka wauguzi na wakunga viongozi kuhakikisha vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinaanzisha na kuimarisha madawati ya huduma kwa mteja ili kuhakikisha kero za wananchi vituoni zinashughulikiwa kwa wakati na kupatikana kwa mrejesho haraka.
Waziri Mhagama ametoa maelekezo hayo leo Aprili 28, 2025 wakati akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa wauguzi viongozi uliofanyika mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo waganga wakuu wa mikoa na halmashauri, waganga wafawidhi wa hospitali za mikoa, wasajili wa mabaraza pamoja na wadau wa maendeleo.
"Nawataka pia, mkafuatilie na kuhakikisha wateja wanapata huduma kwa wakati na kutoa elimu, kwani ni wajibu wa mteja na mtoa huduma, kuimarisha usimamizi wa ndani wa utoaji huduma sambamba na kuimarisha matumizi ya miongozo kwenye utoaji wa huduma kwa kuhakikisha usalama kwa wateja," amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagma amewataka wauguzi viongozi hao kuendelea kusimamia taaluma yao, nidhamu, maadili na ubunifu katika kazi ili kuhakikisha kila mgonjwa anapata huduma bora za afya na zenye staha pamoja na utu kwa kuzingatia usiri baina ya mgonjwa na mtoa huduma.
"Kipaumbele chetu kikubwa kwa sasa kama Wizara ya Afya ni kuimarisha usimamizi wa utoaji wa huduma bora za afya na utendaji kazi wa watumishi mnaowasimamia, ninyi ndio wasimamizi wa nguvu kazi ya sekta ambao wanatoa huduma kwa takriban asilimia 80, niwasihi sana mkayatekeleze kwa ufanisi haya yote mliyoazimia ili kuleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma za afya nchini," amesema Waziri Mhagama
Vilevile, Waziri Mhagama amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Afya imefanya mapinduzi makubwa katika kuboresha huduma za afya kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya majengo, vifaa tiba, upatikanaji wa dawa pamoja na watumishi.