Customer Feedback Centre

Ministry of Health

IDADI YA WAGONJWA WA MOYO NA SHINIKIZO LA JUU lA DAMU YAONGEZEKA KWA 9.4%

Posted on: September 29th, 2023


Na. WAF - Dar es Salaam


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema takwimu za Wizara ya Afya kupitia MTUHA (DHIS -2) zinaonesha kumekuwa na ongezeko la asilimia 9.4 kwa magonjwa ya Moyo na Shinikizo la Juu la Damu pekee kutoka wagonjwa Mil. 2.5 Mwaka 2017 hadi wagonjwa Mil. 3.4 Mwaka 2022.


Waziri Ummy ameyasema hayo leo Septemba 29, 2023 kwenye maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam.


“Takwimu za Wizara ya Afya kupitia MTUHA (DHIS-2) zinaonesha kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa Moyo na Shinikizo la Damu kwa asilimia 9.4”. Amesema Waziri Ummy


Aidha, Waziri Ummy amesema taarifa za ufuatiliaji wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka mwaka 1980 hadi mwaka 2020 inaonesha ongezeko la magonjwa ya Shinikizo la juu la Damu na Kisukari katika jamii kutoka asilimia 1 hadi 9 kwa wagonjwa wa kisukari na kutoka asilimia 5 hadi 26 kwa wagonjwa wa Shinikizo la juu la Damu.


“Magonjwa haya mawili ndiyo chanzo kikuu cha magonjwa ya Moyo, Figo pamoja na ugonjwa wa Kiharusi hivyo ongezeko hili ni tishio kwa ustawi wa Afya ya jamii yetu na ndiyo sababu inatuweka hapa leo kujadili mikakati ya kukabiliana nayo”. Amesema Waziri Ummy


Aidha Waziri Ummy amesema, Magonjwa ya Moyo na ugonjwa wa Kiharusi yanaweza kuzuilika kwa mtu mmoja mmoja na jamii yetu kwa kuweza kuchukuwa hatua za haraka. 


“Kwa mujibu wa maelezo ya wataalam sababu zinazopelekea kuongezeka kwa magonjwa Yasiyoambukiza ikiwemo Magonjwa ya Kiharusi ni pamoja na kutozingatia ulaji unaofaa ambapo kwa nchi yetu inaonesha asilimia 3 tu ya watu wazima wanatumia kiasi cha wastani wa kutosha cha matunda na mbogamboga”. Amesema Waziri Ummy


Hata hivyo, Waziri Ummy amesema idadi ya watu wazima wanaofanya mazoezi ni imeongezeka ukilinganisha na vijana huku akiwasihi kutenga muda Zaidi wa kufanya mazoezi


“Ninawasihi ndugu zangu mtenge muda wa kufanya mazoezi japo dakika 150 kwa wiki na mazoezi haya siyo lazima yawe ya kukimbia yanaweza kuwa hata ya kutembea, kupima Afya japo mara moja kwa mwaka, kupunguza vilevi na kuacha kabisa matumizi ya tumbaku.


Pia Waziri Ummy amesema kupunguza matumizi yaliyokithiri ya chumvi, sukari na mafuta ya kupikia kwa kuzingatia ushauri wa muhimu unaotolewa na madaktari kwa kufanya hivi kutaweza kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo tatizo la Moyo. 


Sambamba na hilo, Waziri Ummy ameitaka Taasisis ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) pamoja na Hospitali za Kanda Maalum kuwajengea uwezo Hospitali zilizo chini ya ngazi zao kwenye mikoa na kanda walizopo kwa kufanya kambi za matibabu za pamoja.


Katika maadhimisho hayo ya Siku ya Moyo Duniani, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Bingwa wa Moyo Nchini (TCS) na kampuni mbalimbali za uingizaji na usambazaji wa dawa za binadamu wanatoa huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa ya Moyo.