Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HUDUMA ZA MAABARA NI MSINGI WA HOSPITALI

Posted on: September 28th, 2023

Na. WAF, Moshi

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel amesema Huduma za maabara ndiyo msingi mkuu wa Hospitali katika kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha.


Dk. Mollel amebainisha hayo Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro wakati akifungua mkutano wa mwaka wa 36 wa Chama cha wataalamu wa maabara nchini ambapo amesema kuwa kiasi cha Shilingi trioni 6.7 kilichowekezwa na serikali ya awamu ya sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya afya nchini asilimi kubwa imelenga kwenda kuboresha Huduma za maabara.


Dkt. Mollel amesema jiwe la msingi katika sekta ya afya ni maabara hivyo serikali itaendelea kuboresha Huduma za maabara katika hospitali zote nchini ili wananchi waweze kupata Huduma bora.


“Hospitali yoyote msingi wake ni maabara ndiyo maana mtaona hivi sasa serikali yetu ya awamu ya sita chini ya uongozi imara wa Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita katika kuwekeza kwenye Huduma za maabara kwa kufunga mashine za MRI, CT Scan na mashine nyine za kupima vimelea vya magonjwa mbalimbali katika hospitali zote nchini” ameeleza Dkt. Mollel


Amesema maabara ni muhimu sana kwani zimekuwa msaada wakati inapotekea mlipuko wa magonjwa mbalimbali na kusaidia kutambua sambuli kwa wakati.


“Tulipamba na UVIKO-19 watu wa maabara ndiyo walikuwa msaada lakini pia tulipambana na homa ya mgunda watu waliokuwa mstari wa mbele ni wataalam wa Huduma za maabara”amesisitiza Dkt. Mollel


Aidha amesema lengo la kongamano hilo ni wataalam wa Huduma za maabara nchini kukaa na kujadili kwa namna gani wataboresha huduma hizo ngazi ya taifa hadi ngazi ya msingi.


Lakini pia wataalam hao wameeleza mambo yao ambayo wanahitaji serikali iwafanyie ili kuboresha huduma hizo za maabara nchini na kuhakikisha Huduma bora inapatikana kwa wananchi wanao wahudumia.


“Mambo yao wataalam hawa tayari yameshanza kufanyiwa kazi tayari kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alishatoa maelekezo ambayo wizara imeanza kuyatekeleza ili kuboresha mambo yao ikiwemo maslahi na mambo mengine”, ameeleza Dkt. Mollel