Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HOSPITALI ZA UMMA NCHINI ZATAKIWA KUNUNUA MAJI TIBA (DRIP) KATIKA VIWANDA VYA NDANI

Posted on: October 12th, 2023

Na. WAF - Dar es Salaam


Serikali kupitia Wizara ya Afya imeelekeza Hospitali zote za Umma kununua Maji Tiba (Drip) katika viwanda vya ndani vinavyotengeneza bidhaa hizo za Dawa hapa nchini ili kuwaunga mkono na kuwavutia wawekezaji wengine. 


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu aliyasema hayo leo Octoba 13, 2033 wakati alipotembelea katika kiwanda cha Alfa Pharmaceuticals kilichopo Mbagala Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam. 


“Nataka kuwahakikishia wazalishaji wa ndani wa dawa hususan Maji Tiba, Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itawalinda, itawalea na itawabeba, hatuwezi tukaacha uwekezaji huu mkubwa mlioufanya ukapotea, tutaendelea kununua Maji Tiba ndani ya nchi”. Amesema Waziri Ummy 


Waziri Ummy ametoa rai kwa Watanzania hususan kwa wenye Hospitali, kuwaunga mkono wawekezaji wa ndani wanaozalisha Bidhaa za dawa hususan Maji Tiba ili kuwavutia wawekezaji wengine kuja kuwekeza nchini.


Katika kutekeleza hilo, Waziri Ummy amesema Serikali imeshaelekeza kwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na kufanya uwamuzi wa kununua Maji Tiba katika viwanda vya ndani ili kuwaunga mkono wazalishaji wa ndani ya nchi kuanzia tarehe 1 Julai 2023.


Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa kiwanda hicho cha Alfa Pharmaceuticals kina uwezo wa kuzalisha chupa za Maji Tiba Mil. 12 kwa mwaka na kiwanda cha Kairuki kinazalisha chupa Mil. 37 kwa Mwaka kwa hiyo viwanda viwili vinauwezo wa kuzalisha chupa Mil. 49 kwa mwaka. 


Waziri Ummy wakati akitoa faida za uwekezaji amesema, kuna faida nyingi za kuzalisha bidhaa za Afya ndani ya nchi ikiwemo kuokoa fedha za Serikali, kupungua kwa gharama za bidhaa hizo pamoja na kupatikana kwa wakati.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Alfa Pharmaceuticals Bw. Bashir Haruni ameihakikishia Serikali kuwa itaendelea na uzalishaji wa bidhaa za dawa (Drip) kwa lengo la kuwahudumia Watanzania. 


“Tutaendelea kuwekeza katika Sekta hii ya Afya na tayari pia tumeshawekeza katika Hospitali, naishukuru sana Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuunga mkono katika jitihada hizi za kuwahudumia Watanzania”. Amesema Bw. Harun