Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HAKIKISHENI TAARIFA ZA TAFITI ZINAKUWA SULUHU YA CHANGAMOTO ZA KIJAMII.

Posted on: November 30th, 2023


NA WAF – MOROGORO 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe ametoa rai kwa wadau na wataalam wa Afya, sayansi na teknolojia nchini kuhakikisha tafiti wanazofanya zitasaidia kuleta suluhisho la changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Afya.

Ameyasema hayo wakati akifunga Kongamano la Kitaifa la Kisayansi lililofanyika Mkoani Morogoro ambapo wadau na wataalamu wa masuala ya sayansi na tafiti walikutana kwa siku mbili kujadiliana kwa pamoja juu ya tafiti mbalimbali, lengo likiwa ni kutoa mwelekeo dhidi ya Maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI.

Dkt. Maghembe amesema Serikali inajivunia wanataaluma hasa wanaofanya tafiti za ndani zitakazoleta suluhisho katika jamii hasa kwenye sekta ya afya,

 “Hakikisheni hizo tafiti mnazofanya ziwekwe kwenye lugha rahisi ambayo kila mtanzania ataelewa nini kimeandikwa na mzisambaze hadi ngazi ya chini kabisa ya serikali za Mitaa ili kusudi kila mtanzania aweze kunufaika na hayo machapisho yenu ya kitaalamu’’.amesema Dkt. Maghembe

Dkt Grace Maghembe amesema kuwa lengo la kongamano lilikuwa ni kukaa kwa pamoja kwa wadau na kujitathimini kazi ya serikali pamoja na wadau wamaendeleo kutekeleza afua za Afya pia kufanya tafiti kwa wakati ilikuona namna ya kutekeleza afua za kudhibiti maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

“kupitia kongamano hili litasaidia serikali kuona kazi zilizofanyika mambo gani yaliyofanyika vizuri na mambo gani ambayo haya kufanyika vizuri na kutuonyesha mambo gani ya kujifunza kutoka taasisi mbalimbali,Aidha kupitia majadiliano haya yatatuwezesha kuandaa sera itakayotekelezwa kwa jamii kwasababu tayari tumeshafahamu nini jamii inahitaji huko ngazi za chini na kwakuwa tayari tumeshapata taarifa za kitaalamu za kitafiti” ameongeza Dkt. Maghembe.

Aidha ameongeza kuwa lazima tupambane ili kuhakikisha kufikia malengo ya 20/30 Kwa kuangalia tumefikia wapi kwenye jitihada za mapambano.

“kuhusiana na changamoto ya kukabiliana na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto lazima iende kwa vitendo, pia kwa upande mwingine tumepiga hatua kubwa kwenye vita vya unyanyapaa lakini bado kuna changamoto kubwa ya unyanyapaa hadi leo watu wanaogopa kujitokeza kujitangaza kuwa anamaambukizi na kuwa hawako huru kuzungumza kwa familia na marafiki na waathirika wanavyokaa kimya ndio kunasababisha kuongezeka kwa maambukizi mapya jambo ambalo linahitaji tafiti za kina kuhusu suluhisho la kupambana na unyanyapaa katika Jamii” amesema Dkt. Maghembe.