Customer Feedback Centre

Ministry of Health

FANYENI KAZI KWA UADILIFU NA UFANISI ILI KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI.

Posted on: November 7th, 2023

Na WAF, Tanga

Naibu Katibu Mkuu wizara ya Afya Dkt Grace Magembe amewataka watumishi wa afya nchini kuwajibika kwa kufanya kazi kwa ufanisi na uwadilifu ili ili kutimiza malengo ya Serikali ya awamu ya sita ya kutoa huduma bora kwa wananchi.


Dkt. Magembe ametoa kauli hiyo wakati wa kikao chake na watumishi wa afya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bombo (Tanga) ambapo amesema watumishi wanatakiwa wajitume katika kuwahudumia wananchi.


 “Wapo baadhi ya watumishi wanaofanya kazi kwa mazoea na wamehusika kwenye vitendo ambavyo ni kinyume na maadili, tutawachukulia hatua kali kwa sababu wanaharibu taswira ya sekta ya Afya”. Amesema Dkt. Magembe


Aidha Dkt. Magembe amekemea vitendo vya utoroshwaji wa wagonjwa na kuwasababishia wananchi gharama zisizo za lazima huku akisisitiza hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa kila atakaebainika.


“Zipo taarifa za baadhi yenu kutorosha wagonjwa kupeleka kwenye hospitali za nje badala ya kuendelea kupata huduma kwenye hospitali za umma na hivyo kuwasababishia wananchi usumbufu na gharama zisizo za lazima, tutashuhulika na wewe". Amesema Dkt Magembe


Hata hivyo Dkt. Magembe amewasisitizia watumishi hao kufanya kazi kwa ushirikiano na kila mmoja awe tayari kujifunza mazuri kutoka kwa mwenzie ili wote wafanye kazi iliyo nzuri. 


"Ni imani yangu hatutasikia wala kuona uzembe wa aina yoyote, bali mtabadilika na kufanya kazi zenu kwa bidii, ubunifu na uweledi mkubwa ili kutimiza malengo ya Serikali ya awamu ya sita ya kutoa huduma bora kwa wananchi wake". Amesisitiza Dkt. Magembe