Customer Feedback Centre

Ministry of Health

DKT. MAGEMBE AKUTANA NA UONGOZI WA KAMPUNI YA ABBOT NCHINI AUSTRALIA

Posted on: July 27th, 2023

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Abbot Mr. Hugo Xi pamoja na Mr. Bruno Mkurugenzi wa manunuzi wa kampuni hiyo wakati wa Kongamano la Kimataifa la UKIMWI lineloendelea mjini Brisbane Australia.

Katika mazungumuzo hayo wamejadiliana kuhusu upatikanaji wa kipimo kilichoboreshwa kutambua maambukizi ya VVU ndani ya siku saba badala ya siku ishirini na moja kama ilivyo kwa vipimo vinavyotumika sasa.

Dkt. Magembe amepongeza hatua hiyo ambayo itawezesha kutambua mapema hali ya maambukizi na wagonjwa kuanza dawa za kufubaza virusi mapema, kuimarika afya, kuepuka magonjwa nyemelezi na kupunguza uwezekano wa maambukizi ya VVU kwa mwenza ikiwa ni hatua muhimu katika kuelekea malengo ya kutokomeza UKIMWI ifikapo 2030.

Aidha wameongelea upatikanaji kwa kipimo cha jipime mwenyewe (HIV self- test kits) kwa kutumia damu ambacho kinaaminika zaidi kwa watumiaji.
Huduma ya kujipima mwenyewe imeongeza mwamko wa wananchi kujipima na kutambua hali zao hususani vijana wa rika balehe na makundi ya walioko kwenye hatari zaidi ya kupata maambulizi ya VVU, na kuongeza idadi ya watanzania wanaojua hali zao za maambukizi na kujiunga na huduma za matunzo ya VVU.

Faida nyingine ya huduma ya jipime ni kupunguza msongamano kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kupunguza muda mrefu kwa wananchi kusubiri vipimo vya VVU.

Halikadhalika, Dkt. Magembe alipata fursa ya kuona teknolojia ya vipimo vya upimaji wa hapo hapo (Point of care) hususani kwa Watoto wachanga, Kipimo cha TB kwa watu wanaoishi na VVU.

“Teknolojia hii ni muhimu katika kupunguza adha ya wagonjwa kusafiri muda mrefu kufuata huduma katika Hospitali kubwa”. Amesema Dkt. Magembe.

Mwisho, Dkt. Magembe amesisitiza kuimarisha ushirikiano ikiwemo kufanya tafiti za pamoja zenye lengo la kuboresha huduma kwa wananchi na kutoa majibu ya changamoto za kiafya zinazowakabili watanzania.

Abbort ni Kampuni ya kutengeneza vitendanishi vya huduma za afya ikiwemo kupima maambukizi ya wingi wa VVU pamoja na kupima maambukizi ya UVIKO 19.