Customer Feedback Centre

Ministry of Health

CHANJO YA HPV YAFIKIA ASILIMIA 95 YA WALENGWA NCHINI.

Posted on: April 27th, 2024



Na WAF - Dar es Salaam 


Serikali imesema asilimia 95 ya walengwa wa Chanjo ya Dozi moja ya HPV ambao ni waschana wenye umri kati ya miaka tisa hadi kumi na nne tayari wamepatiwa chanjo hiyo.


Hayo yamebainishwa na Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo Dkt. Florian Tinuga wakati wa Semina kati ya wanahabari wa Mkoa wa Dar es Salaam na waratibu wa chanjo kutoka wizara ya Afya, Semina iliyofanyika Aprili 27, 2024, kwakulenga kutoa elimu kuhusu Chanjo ya HPV.




"Hadi kufikia Aprili 27, 2024 tayari zoezi la Ugawaji wa chanjo ya dozi moja ya HPV imewafikia ya asilimia 95 ya mabinti wenye umri wa miaka tisa hadi kumi na nne wa Tanzania bara na visiwani tangu kuanza kutolewa kwake Aprili 22, 2024" amesema Dkt. Tinuga


Dkt. Tinuga amesema shabaha ni kuwafikia mabinti Millioni tano wa Tanzania nzima ambapo mpaka sasa zoezi hilo limeonyesha mafanikio makubwa ikiwa ni wiki moja tu tangu kuanza kwake.


"Tulipoanza zoezi siku ya Jumatatu tulilenga kufikia watoto wenye umri wa miaka tisa hadi kumi na nne takribani milioni tano na kwa tanzania nzima Bara na Visiwani ambapo kwa bara ni takribani milioni 4,800,000 na Laki mbili kwa upande wa Zanzibar, ila hadi kufikia tarehe 27, Aprili 2023 tumefikia walengwa kwa asilimia 95" amefafanua Dkt. Tinuga.


Dkt. Tinuga ameongeza kuwa kufanikiwa kwa zoezi hilo kumetoka na maamuzi ya kufanya mabadiliko ya kutoa dozi moja sahihi na kuweza kuwafikia mabinti wengi zaidi ambapo kwa siku ya kwanza pekee walichanja asilimia 27 huku lengo likiwa kila siku kuchanja asilimia 20 ya walengwa.


Dk Tinuga ameongeza kuwa wasichana wenye umri wa Miaka kati ya tisa hadi kumi na nne wapatao 5,028,357 kwa Bara na Visiwani, ikiwa bara ni 4,841,298 na 187,059 Visiwani watafikiwa na chanjo hiyo kwa Mikoa 31 na Halmashauri 195 kabla ya kufikia mwisho mwezi Disemba mwaka huu.


Katika hatua nyingine Dkt. Tinuga amesema, Chanjo hiyo ni salama na hutolewa bure kwa walengwa kwa hiari na husaidia kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya mlango wa kizazi.


"Chanjo HPV inapatikana katika vituo vya kutolea huduma za Afya na kwenye shule na hutolewa wakati wa kampeni na kawaida,” amesisitiza Dk Tinuga.


MWISHO