CHANJO NI AFUA MUHIMU KUJIKINGA DHIDI YA MAGONJWA
Posted on: March 23rd, 2026Na Hassan Kimweri, WAF - Mwanza
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema Chanjo ni afua muhimu kwa wananchi kwa ajili ya kujilinda dhidi ya maradhi mbalimbali.
Dkt. Maghemba ameyasema hayo alipo muwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe, alipokuwa akiongoza Mkutano Mkuu wa kamati tendaji ya kitaifa ya chanjo inayojumuisha viongozi na wadau wa Sekta ya Afya wenye lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa huduma za chanjo nchini.
Katika mkutano huo uliofanyika leo Machi 23, 2026, Dkt. Magembe amesema Chanjo ni afua muhimu katika kujikinga na magonjwa endapo walengwa watakamilisha idadi kamili ya dozi (chanjo) elekezi ili kupata kinga kamili dhidi ya ugonjwa wa Polio, Surua, Kuhara, Kifua kikuu, Saratani, Homa ya ini, Rubela na magonjwa mengine yanayozuilika kwa chanjo.
Aidha, Dkt. Magembe amesema Takwimu za mwaka 2025/26 zinaonesha viwango vya maambukizi ya surua yalikuwa chini ya asilimia 10 kwa watoto waliokamilisha dozi mbili za chanjo ukilinganisha na wale ambao hawakupata chanjo au hawakukamalisha dozi ambao walikuwa ni asilimia 46.9.
Amesema, zoezi la chanjo ya Polio linaloanza mwezi Machi 2026, linahitaji kutangazwa kwa jamii, shuleni, maeneo yote ya mikusanyiko, nyumba za ibada ili wazazi na walezi wapeleke watoto wao kupata chanjo.
Mkutano huo umehusisha Viongozi Wakuu wa Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI na Wadau wa Chanjo wakiwemo WHO, UNICEF, asasi za kiraia na Sekretarieti ya Mpango wa Taifa wa Chanjo.