BIMA YA AFYA KWA WOTE YAANZA KWA KISHINDO, WAZIRI MCHENGERWA ALIAMBIA BUNGE
Posted on: May 11th, 2026Na Atley Kuni, WAF-Dodoma
Serikali imeanza rasmi utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ikiwa ni sehemu ya maboresho makubwa yanayolenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha ikiwa ni mwanzo wa mapinduzi mapya katika Sekta ya Afya nchini.
Hayo yamesemwa Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27, Mei 11, 2026, ambapo amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanaingia kwenye mfumo wa bima ya afya ili kupunguza gharama za matibabu na kuongeza usawa wa upatikanaji wa huduma za afya.
"Serikali itaendelea kusajili wananchi kutoka kaya zenye uhitaji pamoja na wale wenye uwezo ili kuhakikisha huduma za afya zinawafikia Watanzania wote bila ubaguzi", amesema Mchengerwa na kuongeza kuwa mpango huo pia utaenda sambamba na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya.
Waziri Mchengerwa amefafanua kuwa, Serikali imeweka mikakati ya kuimarisha mfumo wa ugharamiaji wa huduma za afya kwa kutumia vyanzo vya ndani pamoja na kuongeza ushirikiano na sekta binafsi ili kuhakikisha mfumo wa bima unakuwa imara na endelevu kwa manufaa ya wananchi.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote utasaidia kupunguza mzigo wa wananchi kutumia fedha nyingi kupata matibabu, huku ukitarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora katika hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa, mafanikio ya mpango huo yatategemea ushiriki wa wananchi pamoja na taasisi mbalimbali kwenye kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga mfumo wa afya wenye usawa na unaomlinda kila Mtanzania dhidi ya gharama kubwa za matibabu.
Serikali inaamini kuwa kupitia utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, Tanzania itaingia katika hatua mpya ya kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa urahisi zaidi, huku wananchi wakiondokana na hofu ya kushindwa kupata matibabu kutokana na changamoto za kifedha.