ZANZIBAR YAVUTIWA NA UBORA WA HUDUMA ZA KIBINGWA HOSPITALI YA BMH
Posted on: June 1st, 2025
NA WAF - DODOMA
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeendelea kuwa miongoni mwa vituo bora vya kutoa huduma za afya za kibingwa nchini, hasa katika eneo la uchunguzi wa picha na matibabu maalum.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Mngereza mzee Miraji akiwa katika ziara kwenye hospitali hiyo Mei 31 2025, ambapo amejionea huduma za hali ya juu zinazotolewa hospitalini hapo kwa kutumia vifaa vya kisasa na wataalam waliobobea katika fani mbalimbali.
Katika ziara hiyo, Dkt. Miraji amepokelewa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. Charles Shija ambaye amemueleza kuhusu mafanikio mbalimbali ya hospitali hiyo tangu kuanzishwa kwake akifahamishwa kuwa BMH imeendelea kuwa kitovu cha huduma za kitaalam nchini, ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma za rufaa, upasuaji wa kibingwa, na matibabu maalum ya magonjwa sugu.
Aidha, Dkt. Miraji ametembelea idara muhimu hospitalini hapo, zikiwemo Idara ya Radiolojia na Idara ya Magonjwa ya Saratani na kuona uwekezaji mkubwa wa vifaa vya kisasa kama mashine za CT Scan, huduma kwa wateja, MRI, pamoja na huduma ya upandikizaji wa uboho (Bone Marrow Transplant), huduma ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa wanaohitaji uchunguzi na tiba ya hali ya juu ndani ya nchi.
Dkt. Miraji ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina nia ya dhati ya kujifunza na kuiga mifumo bora ya uendeshaji wa huduma za afya kama inavyofanyika BMH, ili kuhakikisha kuwa wananchi wa Zanzibar pia wananufaika na huduma bora. Amesisitiza kuwa uwepo wa teknolojia ya kisasa na wataalam waliobobea ni nguzo muhimu ya maendeleo ya sekta ya afya.
Katika mazungumzo yao na uongozi wa hospitali, Katibu Mkuu na ujumbe wake wamejadili kuhusu fursa za kuanzisha makubaliano ya ushirikiano (MoU) kati ya Serikali ya Zanzibar na Hospitali ya BMH kwa lengo kurahisisha uratibu wa mafunzo ya wataalam wa afya, mifumo ya TEHAMA, rufaa za wagonjwa, pamoja na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu na kiteknolojia.