WIZARA YA AFYA, UDOM KUANDAA MWONGOZO HUDUMA ZA UCHUNGUZI WA SONOGRAFIA
Posted on: March 31st, 2026Morogoro
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kupitia Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii (SoNPH), kimewakutanisha wadau wa Sekta ya afya nchini kujadili na kuandaa mwongozo wa huduma za papo kwa papo za uchunguzi wa Sonografia (Point of Care Ultrasound, POCUS).
Akifungua kikao hicho Machi 30, 2026 Mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Huduma za uchunguzi wa magojwa na matengenezo ya vifaa tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt. Alex Magesa amesema, lengo ni kujenga uelewa wa pamoja na kuweka misingi itakayosaidia matumizi sahihi, salama na yenye tija katika ngazi zote za utoaji huduma za afya, hususani katika vituo vya awali.
“Kabla ya mwongozo huu kila mmoja amekuwa akifanya vipimo kwa namna anavyoweza, baadhi tumekuwa tukifanya mafunzo ya Sonografia kwa jinsi tunavyoona inafaa lakini siyo sawa. Hivyo kupitia mwongozo huu, utakapokamilika kila mtaalamu itabidi afanye kazi ya uchunguzi wa Ultrasound kwa kufuata mwongozo unavyotaka”, amesema Dkt. Magesa.
Naye Mhadhiri na Mtafiti Mkuu wa mradi huo kutoka UDOM, Dkt. Leonard Katalambula, ameeleza kuwa juhudi hizo zinalenga kuimarisha ushirikiano wa wadau na kuweka msingi thabiti wa matumizi ya POCUS katika kuboresha huduma za afya nchini.
Kwa upande wake, Msajili wa Baraza la wataalamu wa Rediolojia kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ramadhani Kabala, amesisitiza kuwa, utekelezaji wa mpango huo utaongeza upatikanaji wa huduma za ultrasound katika ngazi za chini na kupunguza ulazima wa wagonjwa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika Hospitali za Rufaa na Mikoa.
"Mradi huu unatekelezwa na UDOM kwa ufadhili wa Gates Foundation, ukiwa na lengo la kuimarisha uwezo wa watumishi wa afya kupitia mafunzo ya matumizi sahihi ya POCUS,"amesema Dkt.Ramadhan
Kikao hicho kimehusisha wadau mbalimbali, wakiwemo wawakilishi kutoka Zanzibar, OWM – TAMISEMI, Mabaraza ya kitaaluma, vyama vya kitaaluma, vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na Vyuo vikuu Nchini.