Wizara Ya Afya

WAZIRI MCHENGERWA: ATOA MAAGIZO MAZITO 6 KUBORESHA UPATIKANAJI WA DAWA NA BIDHAA ZA AFYA NCHINI

Posted on: April 2nd, 2026

Na Abduly Madenge, WAF - Dar es Salaam.


Waziri wa Afya Mhe. Mohammed Mchengerwa ametoa maagizo sita muhimu yenye lengo la kuboresha upatikanaji wa dawa na bidhaa za afya nchini, akisisitiza kuwa wakati umefika wa kuwajibika na kuleta matokeo chanya na  yanayoonekana kwa wananchi.


Akizungumza Aprili 2, 2026 katika Bohari ya Dawa (MSD) jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao chake na Wadau wa dawa na vifaa tiba nchini amesema Serikali haitaridhika na takwimu nzuri zisizoakisi hali halisi ya huduma, akibainisha kuwa, bado wananchi wanakosa dawa licha ya ripoti kuonesha hali ni nzuri.


Katika kuimarisha mfumo huo, Mhe. Mchengerwa ametoa maagizo yafuatayo ambapo Kwanza, amemtaka Mfamasia Mkuu wa Serikali kufanya mapitio ya mfumo wa upimaji wa upatikanaji wa dawa ili kuzingatia si tu uwepo wa dawa, bali pia utoshelevu wake kulingana na mahitaji halisi.


Pili, Mhe. Mchengerwa amemuagiza Mganga Mkuu wa Serikali kusimamia kikamilifu uandishi wa dawa kwa kuzingatia Mwongozo wa Matibabu na Orodha ya Taifa ya Dawa Muhimu, pamoja na kuimarisha Kamati za Tiba na Dawa (MTC).


Tatu, ameagiza kufanyika kwa mapitio ya miongozo na miundo ya usimamizi wa vituo vya afya ili kuhakikisha wafamasia wanakuwa sehemu ya menejimenti.


Nne, Hospitali na vituo vyenye madeni MSD kufanya majadiliana na makubaliano na taasisi hiyo na kuandaa mpango wa kulipa madeni ya Taasisi husika ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa, akisisitiza kuwa hili ni wajibu wa msingi.


Tano, Mhe. Mchengerwa amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri nchini kusimamia kwa karibu matumizi ya fedha, hasa katika ununuzi wa dawa, na kuhakikisha matumizi sahihi ya mifumo ya taarifa.


Sita, wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu changamoto za upatikanaji wa dawa katika maeneo yao.


Aidha, amesema Serikali imeanza mchakato wa kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa uandishi wa dawa (e-Prescription) utakaosaidia kuongeza uwazi, ufuatiliaji na ufanisi, pamoja na kupunguza tatizo la kuandikiwa dawa zisizopatikana.


Amesema, ingawa takwimu zinaonesha upatikanaji wa dawa kufikia asilimia 89 hadi 90, bado kuna malalamiko kutoka kwa wananchi, hali inayoonesha kuwepo kwa pengo kati ya takwimu na uhalisia, hivyo Serikali itaendelea kuchukua hatua kuhakikisha kila mwananchi anapata dawa kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.