Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATAALAM WA MACHO WATAKIWA KUJISAJILI KWENYE MFUMO WA HFRS ILI WAWEZE KUTAMBULIKA

Posted on: March 21st, 2024



Na WAF - Dodoma


Msajili wa Baraza la Optometria nchini Bw. Sebastian Milanzi amewataka wataalam wa macho nchini waliohitimu mafunzo yao kutoka vyuo vya Mvumi Dodoma na KCMC mkoani Kilimanjaro kuhakikisha wanajisajili kwenye mfumo wa HFRS utakao wawezesha wao kutambulika na mifumo ya Serikali.


Milanzi ametoa rai hiyo Machi 22, 2024 jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya wataalam wa Optometria waliohitimu vyuo na wanaotarajia kutoa huduma ya macho yanayofanyika kwa siku moja.



Milanzi amesema uwepo wa Baraza hilo unatambuliwa kupitia Sheria ya Bunge ya Mwaka 2007 ambayo inampa mamlaka Waziri mwenye dhamana kuunda baraza lenye wajumbe 12 watakaosimamia taaluma hiyo.


“Baraza ni ndio chombo pekee nchini chenye dhamana ya kutoa Leseni za wataalam wa Optometria na kuzisimamia, kwa wale waliosoma vyuo vya ndani na nje ya nchi, hivyo kila muhitimu wa kozi hiyo ili aweze kutekeleza majukumu yake lazima apate usajili wa Baraza hilo”. Amesema Milanzi.


Milanzi amefafanua kuwa lengo la sheria ikatumike kudhibiti ubora wa huduma zitolewazo na wataalam hao na kwa mujibu wa kifungu cha 11 juu ya sifa za mtu kupata usajili katika baraza hilo.


Akiwasomea baadhi ya sheria zinazo simamia watoa huduma Naibu Msajili Ramadhani Msuya kutoka baraza hilo, amesema kupitia kifungu cha (5), mtu yeyote atakaye kwenda kinyume ataadhibiwa kwa mujibu wa Sheria zinazo simamia taaluma hiyo.


“Tumezoea kuona watu wanauza miwani mtaani lakini hilo ni kosa kisheria kwani kupitia kifungu cha 40 (1) na adhabu yake inafikia hadi milioni kumi au kifungo cha miaka mitano ama vyote viwili kwa pamoja.


Kwa upande wao wataalam hao, wamesema watakuwa tayari kufanya kazi kwa weledi ili kulinda hadhi ya taaluma.


“Kazi hii ni lazima uwe muadilifu, hivyo nitahakikisha ninatunza siri za mgonjwa nikiwa mtoa huduma niliye hitimu mafunzo yangu ambayo yananitaka kufanya hivyo”. Amesema Bi. Digna Karazoka ambaye ni muhitimu kutoka chuo cha KCMC mkoani Kilimanjaro.


Katika hatua nyingine wataalam hao wametakiwa kulinda maadili na kuwa wazalendo kwa nchi ikiwepo kutopokea rushwa.


Jumla ya wataalam 32 wamepatiwa usajili wa kudumu na jumla ya wataalam 44 wamepatiwa usajili wa muda chini ya uangalizi.



MWISHO