Wizara Ya Afya

WATAALAM WA MAABARA WAENDELEA KUJENGEWA UWEZO WA KUKABILI MAGONJWA YA MLIPUKO

Posted on: April 14th, 2026

Na Atley Kuni, WAF - Tabora

Wataalam wa maabara nchini kutoka mikoa ya Tabora, Shinyanga na Mara wameendelea kupatiwa mafunzo maalum ya namna sahihi ya kuchukua, kufungasha kuainisha na kusafirisha sampuli hatarishi za magonjwa ya mlipuko, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mfumo wa utambuzi na udhibiti wa magonjwa hayo.

Mafunzo hayo ambayo yameingia siku ya pili, yanalenga kuongeza uelewa kwa wataalam wa Afya kuhusu taratibu sahihi za kushughulikia sampuli za magonjwa hatari kama Ebola, Marburg na Mpox, ili kuhakikisha zinawasilishwa salama kwenye maabara zenye uwezo wa kupima magonjwa hayo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Aprili 14, 2026 mkoani Tabora, Mratibu wa zoezi hilo, Bw. Joachim Chacha, amesema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kuwepo kwa changamoto kwa baadhi ya wataalam kukosa elimu sahihi ya uchukuaji na usafirishaji wa sampuli, jambo linaloweza kuhatarisha usalama na kuchelewesha majibu ya vipimo.

Kwa upande wake, Mtaalam wa Maabara kutoka Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii (NPHL) ya Dar es Salaam, Bi. Vumilia Mwalongo, amesema kuwa wagonjwa wengi huanzia kupata huduma katika ngazi ya msingi, ambapo kati ya asilimia 65 hadi 80 ya wananchi hupata huduma za afya, hivyo ni muhimu kuimarisha uwezo wa wataalam wa ngazi hiyo.

Amesema lengo kuu ni kuwawezesha wataalam wapatao 41 kuwa na uwezo wa kukusanya sampuli kwa usahihi pamoja na kuchakata taarifa za magonjwa ili kupata takwimu sahihi kuhusu aina ya magonjwa na maeneo yanayoathirika.

Mara baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo wataalam waliopata mafunzo watawafundisha wenzao katika vituo vyao vya kazi na kuwa mabalozi (championi) wa ukusanyaji sahihi wa taarifa za magonjwa pamoja na kusaidia kuboresha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko

Mratibu huyo ameongeza kuwa zoezi hilo ni endelevu, likianza ngazi ya taifa, mkoa, wilaya na sasa kushuka hadi ngazi ya msingi.

Chacha amefafanua kuwa tayari mafanikio yameanza kuonekana ambapo wataalam wanachukua sampuli kwa usahihi, kuweka utambuzi ipasavyo na kuhakikisha zinawasilishwa kwa wakati, tofauti na awali ambapo baadhi walikuwa hawazingatii taratibu hizo.