Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WANANCHI MANYARA WAHIMIZWA KUJITOKEZA KUPATA HUDUMA ZA MADAKTARI BINGWA

Posted on: June 2nd, 2025

Na, WAF MANYARA.

Wananchi Mkoani Manyara wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma za kibingwa kutoka kwa Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi waliombatana wauguzi bingwa katika Hospitali za halmashauri mkoani humo.

Wito huo umetolewa leo Juni 2, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Mhe. Michael Semindu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Queen Sendiga wakati akiwapokea Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi pamoja na Wauguzi Bingwa 48 wa Rais Samia mkoani Manyara.

Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mhe. Semindu amesema huduma hizo ni adimu hivyo wananchi wanatakiwa kutumia fursa hiyo kujitokeza kuwaona madaktari bingwa na kupata matibabu.

“Huduma hizi ni zawadi ya thamani kutoka kwa Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivyo nawahimiza wananchi wote wa Manyara kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizi adimu, pengine ingewalazimu kusafiri kuzifuata mbali huduma hizo, lakini sasa watazipata karibu na kwa gharama nafuu,” amesisitiza Mhe. Semindu.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Andrew Method, amesema kuwa maandalizi yamekamilika na timu ya madaktari bingwa ipo tayari kuanza kazi katika halmashauri zote.

“Tuna furaha kuwa na Madaktari bingwa pamoja na wauguzi bingwa na bobezi ambao watakuwepo kwa siku sita wakitoa huduma katika halmashauri zetu zote saba (7) katika mkoa wa Manyara, hii ni fursa kwa wananchi kupata huduma za kibingwa hivyo nitoe wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika halmashauri zetu zote,” amesema Dkt. Method.

Kwa upande wake, Dkt. Michael Haule, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, ambaye amezungumza kwa niaba ya madaktari wenzake, ametoa wito kwa wananchi wenye changamoto za kiafya kujitokeza kwa ajili ya kupata huduma.