UZINDUZI MAABARA YA KISASA JKCI KUIMARISHA UCHUNGUZI WAGONJWA WA MOYO NCHINI
Posted on: June 12th, 2026Na Zakayo Mosha WAF-Dar es salaam
Waziri wa Afya Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa (Mb) leo tarehe 12 Juni,2026 Jijini Dar es salaam amezindua Maabara ya kisasa ya Uchunguzi wa Magonjwa ya Moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ikiwa ni hatua na mkakati wa Serikali kupitia Wizara ya Afya kuimarisha Uchunguzi na utoaji wa matibabu kwa Wagonjwa wa Moyo nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo,Mhe.Mohamed Mchengerwa amesema kuwa huduma za afya ni nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla,hivyo Serikali imejizatiti katika kuboresha sekta ya afya kwa kutoa mbalimbali za kisasa ikiwemo ya Wagonjwa wa moyo ambazo zitahakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
"Miaka kumi iliyopita, wengi waliona ndoto ya kuwa na kituo cha kisasa cha huduma za moyo nchini Tanzania kama jambo gumu kufikiwa. Leo tunasimama hapa si kuzungumzia ndoto, bali kushuhudia matokeo ya maono, uwekezaji wa Serikali na juhudi za wataalamu wetu. JKCI imeendelea kuwa moja ya taasisi muhimu zaidi katika mfumo wa afya nchini" amesema Waziri Mchengerwa
Ameongeza kuwa, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kuwa tumaini na tegemeo kwa maelfu ya Watanzania wenye magonjwa ya moyo na imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza utegemezi wa huduma za matibabu ya Moto nje ya nchi yetu.
Aidha, Waziri Mchengerwa ameeleza na kusisisitiza kuwa kupitia JKCI, Tanzania imeweza kujenga uwezo wa kutoa huduma za kibingwa na kibingwa bobezi za moyo, kufanya upasuaji wa moyo, huduma za uchunguzi wa kisasa, mafunzo ya wataalamu na tafiti zinazotambulika kimataifa.
"Leo JKCI si taasisi ya Tanzania pekee; ni taasisi inayohudumia wananchi wa Tanzania na mataifa mengine ya Afrika Mashariki na Kati na imeendelea kujijengea heshima kubwa kama kituo cha ubora katika huduma za moyo" amesema Mhe.Mchengerwa