USHIRIKIANO WA KIKANDA NI MUHIMU KUKABILIANA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA AFRIKA(NCDs)
Posted on: June 23rd, 2026Na Aisha Swahibu, WAF - Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amesema ushirikiano wa kikanda na kimataifa ni nguzo muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watu wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), ambayo yanaendelea kuwa miongoni mwa sababu kuu za vifo na ulemavu barani Afrika.
Dkt. Shekalaghe ameyasema hayo leo Juni 23, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akitoa neno la ya ukaribisho katika Mkutano Mkuu wa Tatu wa Kimataifa wa Kimkakati wa Kikanda wa PEN-Plus (ICPPA 2026), unaowakutanisha viongozi, watunga sera, wataalamu wa afya, watafiti, washirika wa maendeleo na wadau mbalimbali kutoka nchi za Afrika na sehemu nyingine za dunia.
Amesema uwepo wa washiriki hao unaakisi dhamira ya pamoja ya kuimarisha mifumo ya afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kinga, utambuzi wa mapema, matibabu na ufuatiliaji wa magonjwa yasiyoambukiza.
“Magonjwa yasiyoambukiza yanaendelea kuwa chanzo kikuu cha vifo na ulemavu, hivyo yanahitaji hatua za pamoja katika kuzuia, kugundua mapema na kutoa huduma stahiki kwa wananchi,” amesema Dkt. Shekalaghe.
Aidha, ameeleza kuwa mkutano wa ICPPA 2026 ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, ubunifu na mafunzo yatakayosaidia kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kujenga uwezo wa mifumo ya afya na kuharakisha utekelezaji wa afua za kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza katika nchi za Afrika.
Dkt. Shekalaghe amesisitiza kuwa kupitia majadiliano na uzoefu utakaoshirikishwa katika mkutano huo, nchi mbalimbali zitapata fursa ya kujifunza mbinu bora zitakazowezesha utoaji wa huduma za afya zilizo karibu na wananchi, zenye ubora na zinazojumuisha huduma za magonjwa yasiyoambukiza katika ngazi ya huduma za afya ya msingi.
Dkt. Shekalaghe ametoa shukrani kwa Shirika la Afya Duniani (WHO), washirika wa maendeleo na wadau wote waliochangia maandalizi na kufanikisha kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Tatu wa Kimataifa wa Kimkakati wa Kikanda wa PEN-Plus (ICPPA 2026), na kueleza kuwa mchango wao unaendelea kuimarisha jitihada za Afrika katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza