TSH.150,000 KUWEZESHA FAMILIA YA WATU 6 KUPATA HUDUMA ZA AFYA 372 KWA MWAKA KUPITIA BIMA YA AFYA KWA WOTE
Posted on: March 26th, 2026Na Mwandishi Wetu, WAF - Arusha
Shilingi laki moja na nusu (150,000) tu kunufaisha familia ya watu sita na kuwezesha kupata huduma za afya 372 kwa mwaka mmoja kupitia mpango wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote.
Akizungumza leo Machi 25, 2026, mkoani Arusha, katika kikao cha Washitiri wa Elimu kwa Umma kilichoratibiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mratibu wa Elimu kwa Umma wa Mpango huo, Said Makora, amesema mpango huu ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa wote.
Bw. Makora amesema huduma zitakazotolewa katika mpango huu ni pamoja na uchunguzi wa maabara, radiolojia, dawa na vifaa tiba, pamoja na upasuaji mdogo na mkubwa, kuanzia Zahanati hadi hospitali za rufaa za Taifa.
Aidha, Bw. Makora amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeweka vyanzo maalum vya mapato vitakavyokusanya takribani Sh bilioni 201.9 katika mwaka wa fedha 2025/2026 ili kugharamia wananchi wasio na uwezo, huku zaidi ya Sh bilioni 48.2 tayari zimekusanywa katika robo ya kwanza, zitakazonufaisha kaya 276,000.
Ameongeza kuwa mpango huo pia unalenga kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika kwa kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto, pamoja na kudhibiti magonjwa yanayoongoza kuathiri wananchi kama malaria, kifua kikuu, na UKIMWI.
Bw. Makora amesema zaidi ya kaya 931,000 tayari zimetambuliwa kupitia kanzidata ya TASAF, huku Serikali ikilenga kufikia zaidi ya kaya milioni 3.9 zitakazonufaika, huku gharama zao zikigharamiwa kikamilifu.
“Mpango huu unakwenda kubadili maisha ya wananchi kwa kuhakikisha wanapata huduma za afya kwa wakati bila hofu ya gharama,” amesema Makora.
Utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unatarajiwa kuongeza usawa katika upatikanaji wa huduma za afya, kupunguza umaskini unaosababishwa na gharama za matibabu, na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla.