Wizara Ya Afya

TANZANIA YATAKA USHIRIKIANO IMARA WA KIKANDA KUTOKOMEZA MALARIA NA NTDs

Posted on: May 21st, 2026


Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, amesema ushirikiano wa kuvuka mipaka ni muhimu kwenye mapambano dhidi ya malaria na Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDs). Amesema hatua za pamoja zinahitajika kwa kuwa magonjwa ya kuambukiza hayaheshimu mipaka ya nchi.

Mhe. Mchengerwa amesema hayo katika kikao maalum kinachofanyika sambamba na Mkutano wa 79 wa Shirika la Afya Duniani mjini Geneva, amesema jamii za mipakani bado ziko hatarini kutokana na maambukizi ya magonjwa hayo.

Mheshimiwa Mchengerwa amesema karibu asilimia 40 ya mzigo wa NTDs duniani uko Afrika, huku changamoto za uhamaji wa watu, huduma dhaifu za afya na ucheleweshaji wa matibabu zikichochea maambukizi katika maeneo ya mipaka.

"Tanzania inaona ushirikiano wa kikanda kama nguzo muhimu ya kufanikisha kutokomeza magonjwa hayo kwa njia endelevu, aidha, Serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya kwa kuunganisha huduma za NTDs katika mfumo wa huduma za msingi" amefafanua Mhe. Mchengerwa.

Mheshimiwa Mchengerwa amesema uwekezaji katika kutokomeza NTDs una faida kubwa kiuchumi, akieleza kuwa kila dola moja inayowekezwa inaweza kuleta faida hadi dola 25 kupitia ongezeko la uzalishaji na kupungua kwa gharama za matibabu.

Katika mkutano huo, Tanzania imeridhia Hati ya Makubaliano iliyoboreshwa ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda dhidi ya NTDs. Amesema makubaliano hayo yatahusisha uratibu wa pamoja, kubadilishana taarifa za magonjwa kwa wakati na kushirikiana rasilimali pamoja na wataalamu wa afya.

Waziri huyo amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na washirika wa kimataifa na wa kikanda katika kuimarisha huduma za afya, huku akisisitiza umuhimu wa misaada inayokamilisha juhudi za ndani badala ya kuzibadilisha.

Mhe. Mchengerwa amesema Tanzania itaendelea kuongoza juhudi za kikanda ili mipaka iwe daraja la ushirikiano badala ya vizuizi, akibainisha kuwa lengo ni kuona malaria na NTDs zikibaki historia barani Afrika.