Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA BARA, VISIWANI WAINGIA MAKUBALIANO UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: May 11th, 2025

Na WAF, Zanzibar

Wizara za Afya Tanzania Bara na Zanzibar zimeingia rasmi kwenye makubaliano ya ushirikiano ya kuwezesha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Halfa ya kusaini hati ya makubaliano hayo imefanyika katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Afya Zanzibar leo Mei 10, 2025 kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya Tanzania Bara Dkt. Seif Shekalaghe na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Mngereza Mzee Miraji na kushuhudiwa na mgeni rasmi Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla na wananchi.

Miongoni mwa maeneo muhimu yaliyozingatiwa kwenye makubaliano hayo ni pamoja na uandaji wa sera za kitaifa za afya na mifumo ya udhibiti, upangaji na ubunifu wa pamoja wa tafiti za afya na ubadilishanaji wa takwimu, teknolojia, na mbinu za kudhibiti magonjwa na kuhamasisha masuala ya Afya.

Maeneo mengine ni kuratibu masuala ya ununuzi na usafirishaji wa dawa na vifaa vya matibabu, kuimarisha programu za afya ya mama na mtoto, lishe na afya ya uzazi pamoja na kujengeana uwezo kwa Taasisi za Afya na wafanyakazi kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Wizara ya Afya za Tanzania Bara na Zanzibar zimekuwa zikishirikiana katika nyanya mbalimbali za kuwezesha kutoa huduma kwa wananchi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo katika kipindi chote hicho hakukuwa na makubaliano rasmi ya maeneo ya ishirikiano, utiaji saini wa hati ya makubaliano ni hatua kabambe ya kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa Watanzania.