SERIKALI YAZIDISHA KASI YA KUOKOA MAISHA, YATANDAZA HUDUMA ZA DHARURA NA ICU NCHI NZIMA.
Posted on: May 14th, 2026Serikali imewahakikishia wananchi kuwa kifo kutokana na kuchelewa kupata huduma za dharura sasa kinakwenda kubaki kuwa historia, kufuatia mkakati kabambe wa kusogeza huduma za kibingwa za uokoaji maisha karibu na makazi ya watu.
Kauli hiyo imetolewa Mei 14, 2026 mkoani Morogoro na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Erasto Sylvanus, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku tatu kilicholenga kupitia miongozo ya matibabu ya wagonjwa mahututi (ICU) na mafunzo kwa vitendo kwa wataalamu wa afya.
Dkt. Sylvanus amebainisha kuwa tija ya maboresho haya kwa mwananchi ni kupatikana kwa huduma za dharura za uhakika na kwa haraka zaidi. Kupitia ushirikiano na OWM TAMISEMI, jumla ya majengo ya kisasa ya dharura (EMD) 125 yamejengwa, ambapo 86 yapo kwenye ngazi ya msingi (Halmashauri) na 39 kwenye hospitali za rufaa.
"Lengo la Rais wetu ni kuona mwananchi anapopata dharura kama ajali au mshtuko wa moyo, asisafiri umbali mrefu. Serikali imejenga majengo hayo na kuweka vifaa vya kisasa ili huduma ya kwanza ya kuokoa uhai ipatikane hapo hapo alipo," alisema Dkt. Sylvanus.
Dkt. Erasto amesema uimarishaji wa ICU na Vitengo vya Uangalizi Maalum pia umefanyika Katika kuhakikisha wagonjwa wanaohitaji uangalizi mkubwa wanapata huduma bora kuanzia ngazi ya msingi kupitia Hospitali za Halmashauri, Dkt. Sylvanus. Hii inamaanisha kuwa wagonjwa mahututi sasa wanapata huduma bora bila kulazimika kwenda hospitali kubwa za mbali. Ili kutimiza azima ya ubora wa huduma hizo, ni lazima kuwe na wataalamu wenye ujuzi, moyo na maadili makubwa katika kuhudumia wagonjwa ili majengo hayo yasiwe kuta tupu, bali yatafsiri huduma bora zinazoahidiwa na Serikali kwa wananchi.
Dkt. Erasto ameongeza kuwa, vituo maalum vya mafunzo kwa vitendo (emergency care skills lab) vimejengwa na kuwekewa vifaa vya kisasa katika hospitali sita (6) za Muhimbili, MUHAS, BMH, KCMC, Bugando, na Mbeya ZRH) kwa ajili ya kufundisha watumishi namna ya kuokoa maisha kwa vitendo, sambamba na mafunzo ya kutumia vifaa kwa usahihi ili kuokoa maisha.