SERIKALI YARIDHISHWA NA MAANDALIZI YA UTAYARI DHIDI YA EBOLA UKEREWE
Posted on: June 24th, 2026Na Cletus Sanga, WAF – Ukerewe, Mwanza
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe, Dkt. Revocatus Cleophas, amesema Serikali imeridhishwa na kiwango cha utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola wilayani humo, wakati wa mafunzo ya utayari yaliyofanyika tarehe 24 Juni 2026 katika hospitali hiyo kwa wahudumu wa afya.
Amesema mafunzo hayo yamefanyika kati ya Wizara ya Afya kwa kushirikiana na CIHEB kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani, yakiwa na lengo la kuimarisha uwezo wa wataalamu wa afya katika kuzuia, kugundua na kukabiliana na milipuko ya magonjwa hatarishi kama Ebola.
“Tathmini iliyofanyika inaonesha kuwa mifumo ya afya imeimarika katika maeneo ya uchunguzi wa awali wa wagonjwa, ufuatiliaji wa visa vinavyoshukiwa pamoja na uwezo wa kutoa huduma salama kwa wagonjwa wenye dalili za Ebola,” amesema Dkt. Cleophas.
“Tumejipanga kuhakikisha kila mhudumu wa afya anafuata taratibu zote za kujikinga na maambukizi ili kulinda maisha yao na ya wananchi kwa ujumla,” Ameongeza
Amesema pia mafunzo hayo yamewajengea uwezo wahudumu wa afya kutumia vifaa kinga (PPE) kwa usahihi na kuongeza umakini katika hatua zote za utoaji huduma ili kuzuia maambukizi ndani ya vituo vya afya.
“Lengo letu ni kuhakikisha tunakuwa na timu imara inayoweza kuitikia kwa haraka endapo kutatokea tishio lolote la Ebola katika wilaya yetu,” ameongeza.
Kwa upande wake Dkt. Fredrick Myula, Daktari bingwa wa magonjwa ya dharura na maafa kutoka Wizara ya Afya, amesema Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa na kutoa taarifa kwa wakati ili kudhibiti hatari ya milipuko.
Aidha, wahudumu wa afya wameahidi kuendelea kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo na kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo maelekezo yote yaliyotolewa. Bw. Myula alihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kuendelea kwa mshikamano na ufuatiliaji wa karibu wa magonjwa katika jamii.