SERIKALI YAITAKA NIMR KUWA KITOVU CHA UBUNIFU WA AFYA TANZANIA
Posted on: June 9th, 2026Na Clement Robert, WAF – Arusha
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imeendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya sekta ya afya nchini kupitia tafiti zinazosaidia Serikali kufanya maamuzi sahihi na kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa kufungua Kongamano la 33 la Kisayansi la NIMR lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC jijini Arusha Juni 9, 2026, Waziri Mchengerwa amesema katika dunia ya sasa yenye ushindani wa maarifa, tafiti za afya hazipaswi kuishia katika machapisho ya kisayansi pekee bali ziwe chanzo cha ubunifu, teknolojia, bidhaa, ajira na fursa za kiuchumi.
Amesema Serikali inaamini NIMR ya sasa na ya baadaye inapaswa kuwa kitovu cha ubunifu wa afya pamoja na kichocheo cha uchumi wa maarifa nchini Tanzania, huku akisisitiza mafanikio ya NIMR yameendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia ya utafiti wa afya, sanjari na taasisi hiyo kutambuliwa na EDCTP kama moja ya taasisi bora za utafiti barani Afrika.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa NIMR imefanya mageuzi makubwa katika tafiti za afya, ikiwemo kupunguza dozi za chanjo ya kinga ya saratani ya shingo ya kizazi kutoka dozi mbili hadi moja, pamoja na kufupisha muda wa matibabu ya kifua kikuu sugu kutoka miezi 18 hadi kati ya miezi sita na 11.
“Taasisi ya NIMR imeboresha upimaji wa kifua kikuu kwa kutumia sampuli ya kinyesi badala ya makohozi na kufanya tafiti za utoaji dawa za kutibu kichocho kwa watoto walio chini ya miaka mitano pamoja na wale wasiokuwa shuleni, tafiti hizi zimechangia mabadiliko ya miongozo ya matibabu katika ngazi ya kitaifa na kimataifa” amesema Mhe. Mchengerwa
Aidha, kupitia mradi wa PENPLUS, NIMR imefanikiwa kuboresha upatikanaji wa matibabu ya kibingwa kwa magonjwa yasiyoambukiza katika ngazi ya wilaya kwa kutumia matabibu, hali iliyosaidia kupunguza rufaa kwa zaidi ya asilimia 80.