Wizara Ya Afya

SERIKALI YABORESHA MIONGOZO YA KITAIFA YA UTOAJI HUDUMA KWA WAJAWAZITO (ANC)

Posted on: April 14th, 2026

Na Cletus Sanga, WAF - Morogoro

Serikali chini ya Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau ikiwemo MUHAS na AAPH, imeendelea kuboresha miongozo ya kitaifa ya utoaji wa huduma kwa wajawazito ili kuimarisha ubora wa huduma za afya ya mama na mtoto.

Hayo yamesemwa leo Aprili 14, 2026, mkoani Morogoro na Mkuu wa Programu ya Uzazi Salama, Dkt. Phineas Sospeter wakati wa kikao kazi chenye lengo la kupitia na kuboresha miongozo ya kitaifa ya huduma za wajawazito (Antenatal Care) na huduma baada ya kujifungua (Postnatal Care), ikiwa ni hatua muhimu ya kuboresha ubora wa huduma za afya kwa mama na mtoto nchini.

“Serikali inalenga kuhakikisha miongozo inayotumika inakuwa ya kisasa, yenye kuzingatia ushahidi wa kisayansi na inayoweza kutekelezeka kwa ufanisi katika ngazi zote za utoaji huduma,” amesema Dkt. Sospeter.

Dkt. Sospeter amesema hatua hii inalenga kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya kwa mama mjamzito na mtoto mchanga kwa kuweka miongozo iliyo bora zaidi, itakayosaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga na kuongeza ustawi wa mama na mtoto nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Africa Academy for Public Health (AAPH), Dkt. Mary Sando, amesema wadau wataendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha miongozo ya kitaifa ya huduma za wajawazito na baada ya kujifungua inaboreshwa zaidi na kuendana na mahitaji halisi ya wananchi.

Naye, Prof. Andrea Pembe kutoka chuo kikuu Muhimbili (MUHAS), amepongeza juhudi za serikali katika kuboresha huduma za Mama na mtoto, na ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kupanga na kutekeleza afua za mama na mtoto nchini ikiwemo kuboresha miongozo ya utoaji huduma.

Prof. Pembe, ameongeza kuwa ushirikiano huo utawezesha utekelezaji bora wa miongozo ya mama na mtoto katika ngazi zote za utoaji huduma za afya, hususani katika vituo vya msingi, na hivyo kuchangia kuongeza ubora wa huduma na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga.