Wizara Ya Afya

SERIKALI, CIHEB-TANZANIA WAIMARISHA UTEKELEZAJI WA MWONGOZO WA KUKINGA NA KUDHIBITI MAAMBUKIZI KATIKA VITUO VYA AFYA NCHINI

Posted on: April 14th, 2026

Na Cletus Sanga, WAF – Morogoro

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) pamoja na mradi wa Usalama wa Afya Duniani unaotekelezwa na CIHEB-Tanzania, inaendelea kuimarisha na kufuatilia utekelezaji wa Mwongozo wa Kukinga na Kudhibiti Maambukizi (IPC) katika vituo vya kutolea huduma za afya ngazi zote nchini.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 13 tarehe, 2026 mkoani Morogoro na Mratibu kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Joseph Hokororo, wakati wa kikao kazi cha kufanya uchambuzi wa takwimu za kukinga na kudhibiti maambukizi pamoja na kuongeza baadhi ya viashiria katika mfumo wa DHIS2.

Dkt. Hokororo amesema kuwa Serikali imeendelea kusisitiza matumizi sahihi ya takwimu ili kuboresha ubora wa huduma za afya na kuhakikisha mazingira salama kwa wagonjwa pamoja na watoa huduma.

Ameongeza kuwa, matumizi ya mfumo wa DHIS2 yamerahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wakati, kuongeza uwajibikaji wa watoa huduma, na kusaidia ufuatiliaji wa utekelezaji wa miongozo ya kitaifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa mradi wa CIHEB-Tanzania, Dkt. Siril Kullaya, amesema mradi huo unalenga kuimarisha mifumo ya ukusanyaji, uchambuzi na matumizi ya takwimu za IPC ili kusaidia maamuzi sahihi katika kudhibiti maambukizi ndani ya vituo vya afya.

Aidha, Dkt. Kullaya amehimiza umuhimu wa kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa afya katika ngazi zote kuhusu utekelezaji wa mwongozo wa IPC, hatua itakayochangia kuimarisha usalama wa wagonjwa, watoa huduma za afya na jamii kwa ujumla.