MIONGOZO BORA YA MAABARA KUWA CHACHU YA KUIMARISHA HUDUMA ZA VIPIMO VYA MAGONJWA
Posted on: March 24th, 2026Na Emmanuel Malegi, WAF – Kilimanjaro
Miongozo bora ndani ya maabara imetajwa kama chachu ya kusaidia ufanisi wa kazi ikiwemo huduma za vipimo na utoaji majibu sahihi kwa haraka.
Hayo yamesemwa Machi 23, 2026 na Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Epidemiolojia na udhibiti wa magonjwa kutoka Wizara ya Afya Dkt. Vida Mmbaga wakati akifungua kikao kazi cha kuandaa mikakati ya upimaji wa vimelea vya magonjwa ya Dengue, Kimeta na Brucelosis kinachoendelea mkoani Kilimanjaro.
Dkt. Vida amesema kuwepo kwa mikakati hiyo kunasaidia na kutoa miongozo kwa wataalam wa Maabara kutojifanyia vipimo kiholela kwa kutumia njia wanazopenda badala yake ufanisi wa kazi utapimwa kwa kufuata miongozo iliyowekwa.
“Kuwepo kwa miongozo hii kutasaidia upimaji wa ufanisi wa kazi ikiwemo kuzuia, kukinga pamoja na kudhibiti magonjwa mbalimbali kwa ufanisi, hivyo miongozo hii inatakiwa kutolewa mapema ili iweze kufuatwa na kusaidia kuboresha huduma za afya nchini”, amesema Dkt. Vida.
Aidha, ameongeza kuwa endapo miongozo hiyo ikikamilika inatakiwa itumike katika ngazi zote za vituo vya kutolea huduma za Afya kuanzia msingi hadi Taifa, lengo likiwa ni kuwa na aina moja ya huduma za Maabara kwa mwananchi sehemu yoyote atakayokwenda.
Kikao kazi hicho kimejumuisha wataalam kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ambapo kwa pamoja wamekusudia kutoka na toleo la kwanza la mwongozo huo kwa ajili ya hatua inayofuata.