MAFUNZO SHIRIKISHI SEHEMU YA KAZI YAIMARISHA HUDUMA ZA DHARURA, AJALI NA WAGONJWA MAHUTUTI NCHINI
Posted on: May 19th, 2026Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha Dharura na Maafa kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI pamoja na wadau mbalimbali, inaendelea kuimarisha huduma za dharura, ajali na wagonjwa mahututi nchini kupitia usimamizi shirikishi na mafunzo ya sehemu ya kazi kwa watumishi wa afya.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 19 Mei, 2026 na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dkt. Daniel Nkungu wakati wa usimamizi shirikishi pamoja na mafunzo ya sehemu ya kazi katika Mkoa wa Morogoro.
Dkt. Nkungu amesema mafunzo hayo yanatolewa kwa watumishi wanaohudumu katika Idara za Dharura na Ajali (EMD) pamoja na Wagonjwa Mahututi (ICU) kwa lengo la kuongeza ujuzi, ufanisi na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wagonjwa.
Aidha, amesema kupitia mafunzo ya vitendo sehemu ya kazi, watumishi wa afya wanapata nafasi ya kujengewa uwezo na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu ili kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini.
Kwa upande wake Afisa Muuguzi kutoka Wizara ya Afya, Bi. Theresia Haule amesema Zoezi hili la mafunzo shirikishi ni mwendelezo wa shughuli zilizokwisha kufanyika katika mikoa ya Pwani, Simiyu, Mara, Tanga na Kigoma, huku kwa sasa likiendelea katika Mkoa wa Morogoro katika Hospitali ya Mkoa pamoja na hospitali za wilaya,” amesema Bi. Haule.
“Wizara inaendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali za afya katika kuhakikisha huduma za dharura na wagonjwa mahututi zinaendelea kuimarika kwa manufaa ya wananchi,” amesema Bi. Haule