Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA SAMIA WAASWA KUTOA HUDUMA KWA WELEDI

Posted on: May 12th, 2025

Na WAF – Kilimanjaro


Madaktari bingwa wa Rais Samia wanaoanza kutoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi mkoani Kilimanjaro wameaswa kutoa huduma hizo kwa weledi katika vituo walivyopangiwa ili kutatua changamoto za kiafya kwa wananchi wanaofika kupata huduma hiyo.


Wito huo umetolewa Mei 12, 2025, na Mganga Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Jairy Khanga wakati akiwakaribisha Madaktari Bingwa hao watakaotoa huduma katika Hospitali za Halmashauri sita za mkoa wa Kilimanjaro.


“Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameanzisha zoezi hili la utoaji huduma za kibingwa kwa lengo la kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi ili kuwafikia wananchi sehemu walipo, hivyo nawasihi sana mtakapokua huko mtoe huduma kwa weledi huku mkiwafundisha wataalam mtakaowakuta ili nao wapate ujuzi na kuboresha utoaji wa huduma katika maeneo yao”, amesema Dkt. Jairy.


Aidha, Dkt. Jairy ameongeza kuwa Hospitali nyingi za Wilaya Mkoani Kilimanjaro bado hazina Madaktari Bingwa hali ambayo inasababisha wananchi kusafiri umbali mrefu na kutumia gharama kubwa kufuata huduma hizo, hivyo uwepo wa Madaktari hao itakua nafuu kwa wananchi na amesisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi.


Naye, mratibu wa ubora wa huduma za tiba kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Pius Kagoma ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha zoezi la Madaktari Bingwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao hivyo ametoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika vituo ambavyo madaktari hao watakua wanatoa huduma.


Mkoa wa Kilimanjaro umepokea jumla ya Madaktari bingwa na Bobezi 43 ambao watatoa huduma mbalimbali kama huduma za afya ya uzazi mama na mtoto, huduma za pua, koo na masikio, huduma za upasuaji, usingizi na ganzi, huduma za magonjwa ya ndani pamoja na huduma za kinywa na meno ambazo zitatolewa kwa siku saba katika Hospitali zote za Wilaya.