MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA MKOANI MTWARA IWE FURSA KWA WANANCHI KUPATIWA MATIBABU.
Posted on: June 2nd, 2025
NA WAF-MTWARA
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, CPA Bahati Geuzye amesema kuwa ni wakati sahihi kwa viongozi wa mkoa wa Mtwara kuhakikisha ujio wa Madaktari Bingwa wa Rais Samia kuwa ni fursa kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mtwara wenye changamoto za kiafya kupatiwa Matibabu.
CPA Bahati amesema hayo leo Juni 02, 2025. wakati wa mapokezi ya madaktari bingwa 63 wa Rais Samia ambao wamefika kutoa huduma kwa wananchi katika halmashauri tisa(9) za mkoa wa Mtwara kuanzia Juni 2-7, 2025.
“Tunamshukuru sana Mhe, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutuona kwa mara nyingine sisi kama wana Mtwara kwa awamu ya tatu tunapokea timu ya madaktari bingwa wa Mama Samia, amefafanua CPA Bahati.
Ameeleza kuwa Mhe Rais amefanya Uboreshaji mkubwa wa huduma za afya mkoani Mtwara ikiwemo uwepo wa hospitali kubwa na ya Kisasa ya Kanda ya Kusini , ongezeko la vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Ligula na Hospitali zote katika ngazi ya chini, sambamba na ajira kwa watumishi wa afya zaidi ya 587 katika mkoa huo.
Kwa Upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Dkt. Benedicto Ngaiza ameeleza kuwa madaktari bingwa wa Magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya ndani, wanawake na uzazi, magonjwa ya watoto, magonjwa ya upasuaji, wataalam wa ganzi na usingizi sambamba na waauguzi bobezi watagaiwa katika halmashauri zote tisa (9) za mkoa wa Mtwara.
“Ujio wa wataalam kwetu itakuwa ni fursa ya kutoa huduma kwa wananchi lakini pia ni fursa ya mafunzo na kuongeza ufanisi kwa watumishi wa afya katika ngazi ya msingi, kwa hiyo kwa upekee nimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta wataalam hao ikiwa ni kwa awamu ya tatu,” amesema Dkt Benedicto Ngaiza.