Wizara Ya Afya

KCMC YAPATA TIBA MIONZI: SERIKALI YAWEKEZA BILIONI 5.5 KUSOGEZA HUDUMA ZA SARATANI KARIBU NA WANANCHI

Posted on: June 24th, 2026

Na John Mapepele, WAF – Kilimanjaro

Tanzania imeandika ukurasa mpya katika mapambano dhidi ya saratani baada ya Serikali kuzindua rasmi Jengo la Tiba Mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC), hatua inayotarajiwa kuwanufaisha maelfu ya wagonjwa wa Kanda ya Kaskazini na nchi jirani.

Uzinduzi huo uliofanyika leo Juni 24, 2026, umeelezwa kuwa moja ya mafanikio makubwa ya uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya, hususan katika kuimarisha huduma za kibingwa na bobezi nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, kabla ya kumkaribisha mhe Rais Samia Suluhu hassan, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (Mb.), alisema jengo hilo siyo tu uwekezaji wa miundombinu, bali ni ishara ya matumaini mapya kwa wagonjwa wa saratani na familia zao.

"Leo tunashuhudia mageuzi makubwa katika mfumo wa afya wa Tanzania. Hili si jengo la kawaida; ni hatua ya kuokoa maisha, kupunguza maumivu na gharama kwa wananchi wetu," alisema Waziri Mchengerwa.

Alibainisha kuwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeweka kipaumbele katika kusogeza huduma za matibabu karibu na wananchi ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa, Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 5.5 katika ujenzi wa jengo hilo pamoja na ununuzi wa sehemu ya vifaa vya tiba mionzi.

Alisema huduma za tiba mionzi katika KCMC tayari zimeanza kutolewa tangu Februari mwaka huu, huku kituo hicho kikiwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 1,100 kwa mwaka katika awamu ya sasa.

Aidha, baada ya kukamilika kwa awamu zote za mradi, kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia hadi wagonjwa 3,900 kwa mwaka, hatua itakayopunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa wagonjwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kupunguza gharama za matibabu kwa familia nyingi.

"Huduma ya karibu kwa mgonjwa wa saratani si suala la miundombinu pekee. Ni suala la matumaini, ni tofauti kati ya kuchelewa na kuwahi kupata matibabu, na wakati mwingine ni tofauti kati ya