HUDUMA ZA KIBINGWA NA BOBEZI ZIMEIMARIKA NCHINI
Posted on: March 27th, 2026Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali imeendelea kuimarisha huduma za kibingwa na ubobezi nchini kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya hospitali, vituo vya afya na ununuzi wa vifaa tiba na dawa vinavyoongeza ubora wa uchunguzi na tiba.
Mhe. Mchengerwa amebainisha hayo leo, Machi 28, 2026, wakati wa mkutano na madaktari bingwa pamoja na wataalamu wa afya, jijini Dar es Salaam
Mhe. Mchengerwa amesema juhudi hizi ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kibingwa ndani ya nchi bila kulazimika kwenda nje, jambo linalopunguza gharama na muda kwa wananchi.
Mhe. Mchengerwa Amebainisha kuwa hatua hizi zinajumuisha kuimarisha hospitali za rufaa za kitaifa, kanda na mikoa, zikiwemo MOI, JKCI, Ocean Road, Benjamin Mkapa, Bugando na KCMC, ambapo vifaa vya kisasa kama CT Scan, MRI, Angio Suite, Mammography na Hyperbaric Chamber sasa vinapatikana kwa wingi na ubora wa hali ya juu
Waziri Mchengerwa amesema kuwa Serikali pia inahamasisha kuendeleza taaluma za madaktari bingwa na wataalamu wengine wa afya kupitia mafunzo maalum, ushirikiano na wadau wa sekta ya afya, ili kuongeza ujuzi na ubora wa huduma zinazotolewa.
Aidha, ameongeza kuwa jitihada za Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kibingwa kwa urahisi bila kulazimika kusafiri umbali mrefu au kwenda nje ya nchi, jambo linalolenga kupunguza mzigo wa kifedha na muda kwa wananchi.